SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumamosi, 11 Februari 2017

T media news

Lusinde Amshukia Mbunge wa BUNDA


Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde amesema kitendo alichofanya mwenzake wa Bunda kupitia chama hicho, Boniface Getere kugawana muda na mbunge wa Serengeti (Chadema), Marwa Ryoba ni utovu mkubwa wa nidhamu.

“Wapinzani hawajawahi hata siku moja kutoa dakika zao kwa CCM. Unampa dakika zako tano mtu ambaye kazi ya chama anachokiwakilisha ni kuikosoa Serikali tu hata katika mazuri si sahihi?” amehoji Lusinde.

Lusinde ni mmoja wa wabunge wa CCM waliomshukia Getere kumpa dakika tano Ryomba ili aweze kuchangia taarifa za kamati za Bunge; Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii na ya Kilimo, Mifugo na Maji baada ya mwenyekiti wa Bunge, Mussa Hassan Zungu kumruhusu azungumze kwa dakika kumi.

“Duniani kote kazi ya upinzani ni kuipinga Serikali iliyopo madarakani na kazi ya wabunge wa chama tawala ni kuishauri Serikali na kuipongeza pale inapofanya vizuri. Hizi ni kambi mbili tofauti,” amesema Lusinde.

Hata hivyo, mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea amesema haoni ubaya kwa mbunge wa CCM kumpa muda mbunge wa upinzani, bali anachokiona CCM wanahamishia kampeni bungeni.

Katibu wa wabunge wa CCM, Jason Rweikiza amesema ni makosa makubwa kwa mbunge wa CCM kutoa muda wake kwa upinzani.

“Si sawa kabisa. Wabunge wengi wa CCM walitamani kuchangia, lakini muda hauruhusu. Tutalijadili hilo kwenye vikao vya chama,” amesema Rweikiza.

Hata hivyo, alipoulizwa Getere iwapo haoni kama amefanya makosa kumgawia mbunge wa upinzani, ametaka kufahamu ni wabunge gani wanaomlalamikia, akisema hajaona madhara yoyote kwa kitendo chake hicho.