SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumamosi, 31 Desemba 2016

T media news

SIMULIZI FUPI: UCHI WANGU UMENIPONZA



NIKAJIWEKA katika kundi la warembo wasioshikika baada ya wanaume kadhaa kunisifia kuwa mimi ni mrembo haswa!!

Shilingi zao zikazidi kunipanda kichwani na kunifanya niwe na kiburi ambacho sikujua kama ni kiburi hadi mama yangu aliponiweka kitako na kunitamkia wazi kuwa hapendezwi na tabia zangu.

Amini! Sikujua kama nimebadilika na kuwa na tabia mbovu, ningeziona vipi kama nilikuwa nazipenda na marafiki wananisifu kila wakati??
Waalimu walikuwa wa kwanza kuniwania, mkuu wa shule akafanikiwa na hatimaye akaitoa bikra yangu nikiwa kidato cha pili tu!
Matokeo yangu yakawashangaza wazazi wangu, usiku sisomi lakini matokeo yangu yalikuwa mazuri. 
Uchi wangu uliyaleta matokeo haya, mkuu wa shule alinipa ahadi hii kuwa nitakuwa nafanya vizuri katika masomo yangu yote. 
Ilikuwa shule binafsi bila shaka waalimu walitii alichowaamuru.
Hatimaye akanijaza mimba, sikujua kama ni mimba hadi dada mkuu aliponivuta kando na kunieleza kuwa nina kila dalili ya mimba.
Nikamwendea mkuu wa shule na kumweleza kuwa nina ujauzito. Akaniruka maili mia na kudai kuwa kuna mwanafunzi nina mahusiano naye ndiye aliyenipachika mimba ile. Nilibaki kinywa wazi nisiamini anachonieleza.
“Na ole wako unyanyue kinywa chako kichafu kumweleza mtu yeyote kuwa mimi nimewahi kufanya zinaa na wewe… unaiona hii…” akatoa kitu ambacho huwa nakiona kwenye filamu tu.
Bunduki!!
“Nakuua sekunde ileile utakayothubutu!!” akamalizia na kisha akanifukuza ofisini mwake.
Kimbilio langu lilikuwa kwa dada mkuu, nilitamani kumweleza kuwa mkuu wa shule anahusika na ile mimba lakini lile onyo likanisuta nikanywea.
Baada ya juma moja dada mkuu akaninong’oneza kuwa kuna zoezi la kupima mimba litapita hapo shuleni. Dada mkuu akanishauri nitoe ile mimba.
Kufikia hapo nikanywea na kusahau kabisa juu ya ule uzuri.
Daktari alitaja kiasi kikubwa cha pesa ambacho sikuweza kukimudu.
Alipoona hivyo akadai kuwa anaweza kunisaidia lakini iwapo nami nitamsaidia.
Akadai anahitaji uchi wangu!!
Kwa mara nyingine nikaishusha sketi yangu daktari afanye awezavyo, akafanya bila huruma na kisha akanitoa ile mimba bila matatizo.
“Tusijuane baada ya hapa… ama tuseme hivi, sijawahi kukutana na wewe sawa!!!” alinionya wakati akiniaga.
Nikajiuliza mara mbilimbili, wanaume ni watu wa namna gani?
Na ni kitu gani hasa wanataka kwangu!!
Uchi tu!! Hakuna mapenzi.
Kama uchi ulinipa maksi nzuri darasani, kisha uchi ukalipa gharama za kutoa mimba!!!
Huu uchi una nini? Nikajiuliza huku nikirejea nyumbani.
Hiyo ilikuwa siku yangu ya kwanza kabisa kuuvaa moyo mgumu kabisa wa kike na kuamua kuishi kulingana na mazingira.
Uchi unaweza kubadili maisha yangu!!

*****

NILIJIDANGANYA KUMBE!!!

Sikujihusisha na wanafunzi wasioweza kuununua uchi wangu kwa bei ninayotaka mimi.
Nikazikubali ofa mbalimbali, wakati huu nilijua kuzihesabu siku zangu na nilijua kumlazimisha mwanaume kuvaa kondomu. Urembo wangu ulinipa kiburi sana.
Kiburi cha wakati huu kilikuwa maradufu, kifo cha baba mzazi kikawa ahueni. Mama hakuwa mkali sana, pia alikuwa na matatizo ya miguu hivyo hakuweza kufuatilia nyendo zangu.
Akiba yangu ndani ikawa kubwa, sikuwapa waalimu uchi ili wanipe maksi nzuri, niliwapa pesa ili wanipe majibu. Na kamwe hawakuzikataa!!
Matokeo yakazidi kumfurahisha mama. Akazidi kunipenda huku akidai kuwa mimi ni mkaidi lakini nina akili darasani.
Ubaya wa jiji la Dar na maeneo mengi Tanzania, kuna msemo wa mtoto wa mwenzio si mtoto wako, hata majirani walioniona nikiwa na mabwana watu wazima hawakumweleza mama. Hivyo alibaki gizani tu.

HAKUNA SIRI CHINI YA JUA!!

Siku hiyo usiku nilikuwa katika hoteli ya kifahari nikiwa na mwanaume aliyekuwa na pete kidoleni. Nilimdanganya mama kuwa nitalala kwa rafiki yangu kwa ajili ya kujiandaa na mtiihani ambao ulikuwa umekaribia lakini ukweli ni kwamba nilikuwa naenda kulala na mwanaume ili nipate pesa ya kununua mtihani.
Nd’o kwanza tulikuwa tumetoka kuoga huku nikimwendesha kama mkewe wa siku nyingi kabisa naye alitii. Tulipopanda kitandani mlango ukagongwa.
Nikiendelea kuchukua utawala mle ndani nikamwambia ni mimi naenda kufungua ule mloango. Nikaufikia bila kuuliza nani yu mlangoni. Nilikuwa na kanga tu mwilini.
Nilipoufungua mlango mara chumba kikavamiwa na watu waliokuwa wameficha nyuso zao. Walikuwa wanaume, mmoja akanirukia na kunipiga ngumi nikaanguka chini, akaniziba mdomo, yule mwingine akamrukia yule mwanaume.
“Waume za watu ni sumu sawa!!” yule aliyekuwa amenikaba alininong’oneza, mapigo ya moyo yalikuwa juu sana.
Kisha likatokea tukio ambalo halitaki kufutika akilini. Yule mwanaume mwingine akatoa kisu na kulididimiza katika shingo ya yule bwana. Damu ikaruka juu akaanza kufurukuta.
Nilitamani nisione lakini yule aliyekuwa amenikaba alinishika kichwa imara na kunitazamisha katika tukio.
Baada ya hapo ikafuata zamu yangu.
Wakatoa nyembe na kuanza kunichanja huku wakiendelea kuniziba mdomo, walinichanja hovyo, mwili wangu mweupe ukalowa damu nilishuhudia jinsi damu ilivyotapakaa mle ndani. Na kisha kiza kikatanda……
Nilikuja kuzinduka na kujikuta hospitali nikiwa na bandeji mwili mzima.
Nilikaa mwezi mzima hospitali, mama alikufa kwa presha baada ya kuambiwa nimefumaniwa na mume wa mtu.
Mke wa marehemu hakuonekana tena mjini bila shaka ni yeye aliyeandaa fumanizi na mauaji ya mumewe.
Nilijiuliza sana ni kwanini mimi aliniacha hai…..
Swali langu lilipata jibu baada ya kuanza kujitazama kwenye kioo. Nilikuwa natisha sana, sikuamini kama ni mimi.
Na kama nilikuwa najitisha mwenyewe vipi watu wengine.
Utu wangu ukakosa thamani hakuna aliyekuwa na muda na mimi tena mtaani.
Kila mtoto mwenye tabia mbaya akatolewa mfano kwangu. Maisha yangu yakaharibika sana, nikawa mtu wa kukataliwa tu kila sehemu! 
Hakuna anayenijali tena… na kwanini wanijali iwapo mwenyewe nilishindwa kujijali wakati nilipokuwa na nafasi ya kufanya hivyo!!!
Sina wa kumlilia, najililia mimi na uchi wangu. 
Makini Recho mimi, UCHI WANGU UMENIPONZA!!!

FUNZO:
Usiugeuze uchi wako biashara!!!
Wasichana wengi waliobalehe wana kasumba ya kujigeuza vifaa vya biashara . 
Tafadhali fursa zipo nyingi, acha kuwa mzembe…. uchi huu unaouona biashara ipo siku utakuponza.
Utakuletea UKIMWI….. UTAKUUA KABISA!!!

MWISHO!!!