Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) umelitaka Jeshi la Polisi mkoani Arusha kuwafikisha mahakamani wanachama wake wanne linaowashikilia kwa siku 12 sasa.
Mtandao huo umedai kuwa watu saba wilayani Longido wanatuhumiwa kutoa taarifa kwa mwanahabari wa Sweden, Susana Nurduland ambaye anafuatilia kwa karibu migogoro ya ardhi wilayani humo.
Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa alisema uendeshaji wa madai hayo umegubikwa na upendeleo wa wazi jambo lililo kinyume na matakwa ya sheria za nchi kwa watuhumiwa wa makosa ya jinai.
“Hadi sasa watetezi wanne wamenyimwa dhamana wakati wengine wenye nafasi za kisiasa wamepewa. Hii si sawa,” alisema Olengurumwa.
Aliwataja walionyimwa dhamana kuwa ni Samwel Nangiria, Supuk Olemaoi, Clinton Kairung na Yohana Mako wakati walioachiwa ni mbunge wa zamani wa Ngorongoro, Mathew ole Timan, Diwani wa Ololosokwani, Yanick Ndina Timan na Mwenyekiti wa Kijiji cha Mundoros, Joshua Makko.
Alieleza kuwa watetezi hao wamenyang’anywa vitendea kazi vyao pamoja na vifaa vya mawasiliano zikiwamo simu za mkononi na kompyuta mpakato.
Wakili wa Kujitegemea wa kampuni ya Law Guards Advocates, Jebra Kambole alisema hiyo ni kinyume na sheria zinazosimamia haki za binadamu nchini.
“Kumshikilia mtu muda mrefu bila dhamana pamoja na kunyimwa uwakilishi ni kinyume na Katiba ya nchi. Ni kinyume na Azimio la Umoja wa Mataifa la Watetezi wa Haki za Binadamu la mwaka 1998,” alisema Kambole baada ya kueleza kuwa watuhumiwa hao wamenyimwa haki ya kuwatumia mawakili.
Licha ya ombi hilo kwa Polisi,mwanachama wa mtandao huo, Rose Sarwatt alimuomba Jaji Mkuu kuingilia kati suala hilo ili kuhakikisha haki inatendekea.
Aliziomba asasi za kimataifa kukemea na kuishauri Serikali juu ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaoendelea huko Loliondo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alisema jeshi lake linasimamia na kutekeleza sheria za nchi na halichagui wa kumkamata kama amefanya kosa la jinai.
“Lazima ukamatwe labda uwe na kinga. Hata mimi, japo kazi yangu ni kukamata lakini nikifanya jinai nitakamwa tu,”alisema na kubainisha kuwa taratibu zinaendelea kuzingatiwa na zikimalizika, watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani.