Mwenyekiti wa zamani wa klabu ya Simba Ismail Aden Rage, naye pia alikuwepo uwanja wa Bandari kwenye game ya nusu fainali ya Ndondo Cup kati ya Kauzu FC dhidi ya Misosi na baada ya mechi hiyo kumalizika alizungumza na waandishi wa habari ambapo alisema anashangaa kwanini vilabu vikubwa vya VPL vinahangaika kwenda nje kusajili wakati hawaonekani kwenye michuano kama Ndondo kuangalia vipaji.
Rage ameshangazwa na uwezo mkubwa unaooneshwa na wachezaji wa Ndondo na kuhoji ni kwanini baadhi yao hawapo kwenye vilabu vikubwa vinanyocheza ligi kuu.
“Nashindwa kuelewa hizi timu zetu kubwa nadhani mnanielewanamaanisha kitu gani, wanatakiwa kuja hapa na kuangalia. Kwa mfano kunawachezaji wengi wenye viwango vya juu ambao hawachezi ligi kuu lakini wanauwezo wa kucheza vilabu vikubwa kabisa,” alisema Rage ambaye alitoa alitoa shilingi 50,000 kwa mchezaji atakayefunga goli la kwanza ndani ya dakika 90. Lakini mchezo huo ulimalizika kwa suluhu hivyo akaikabidhi kwa waandaji ili apewe mchezji atakayeweza kufanya hivyo kwenye mechi ya fainali.
“Sioni haja ya watu kuhangaika kwenda nje ya nchi, wanasajili wachezaji kuto kwa kuangalia nchi walizotoka bada ya kuangalia uwezo wao.”
Mwenyekiti huyo wa zamani wa Chama cha soka Tanzania wakati huo (FAT) hakuacha kumpongeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa dhamira yake ya kuboresha viwanja vitatu kila mwaka ili kufanya wachezaji wa Ndondo wacheze kwenye mazingira bora zaidi na kuyapa heshima na hadhi mashindano hayo.
“Nimpongeze mkuu wa mkoa ambaye ameonesha ushirikiano mkubwa. Kikubwa kilichonifurahisha ameahidi kuboresha viwanja kwa ajili ya mashindano yajayo. Ukishakuwa na viongozi wanaojua mapenzi ya wananchi, hao ndio wa kuwaombea Mungu awajalie kila siku,” alisema Rage.