SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Ijumaa, 2 Machi 2018

T media news

Matumizi ya rejeta kwenye gari na namna ya kuitunza idumu

Rejeta ni kifaa muhimu katika mfumo wa upoozaji wa injini ambapo kinatumika kupoozea maji. Katika ufanyaji kazi wake, rejeta inaundwa na vitu mbalimbali kama vile tanki la juu, tanki la chini, mfuniko (radiator cap), mirija ya kusafirisha maji kutoka tanki la juu kwenda tanki la chini (radiator tube) na njia za wazi za kusafirisha joto (radiator fins).

Wakati wa upoozaji wa injini, kimiminika (coolant) husukumwa kutoka kwenye rejeta na kuingia kwenye injini na kuchukua joto na kutoka nalo kupitia kwenye bomba la mpira (water hoses) na kurejea kwenye rejeta kwa upoozaji.

Kazi ya kwanza ya rejeta ni kuhifadhi maji ya kupoozea injini, na kazi ya pili ni kurahisisha upoozaji wa maji hayo pindi yanaporejea kutoka kwenye injini.

Miongoni mwa mambo yanayofanya rejeta ifanye kazi yake kwa ufasaha ni pamoja na namna lilivyoundwa, eneo lake na unene wa vibomba vinavyopitisha maji, kiasi cha maji kinachopita kwenye hiyo rejeta na kwenda kwenye injini na kiasi cha joto la hewa inayopita kwenye rejeta na kupooza kimiminika kilichomo humo.

Makundi ya rejeta

Rejeta zimegawanyika katika makundi mawili, kundi la kwanza ni lile la maji ya kutiririka kwa ulalo (cross-flow radiator). Aina hii, maji huingia ama kupitia upande wa kulia au kushoto na kutokea upande mwingine.

Kundi la pili ni lile ambalo maji hutiririka kutoka juu ya rejeta kwenda chini kupitia kwenye mirija iliyomo ndani ya rejeta.

Katika hali ya kawaida, rejeta ina njia ya kutolea maji (drain cock), vile vile, rejeta hutumika kupoozea oil ya automatic transmission (automatic gear box).

Oili hiyo huletwa kwenye bomba la mpira au metaliki, na hupita upande wa chini wa rejeta na kupooza maji maji yaliyokwisha poa na kurejesha tena kwenye gia box kuendelea na kazi.

Mambo ya kuzingatia katika matumizi ya rejeta

Ili kusudi rejeta iendelee kufanya kazi vizuri ni lazima kimiminika kinachowekwa kwenye injini kiwe maalum (coolant) kwa kazi hiyo ya kupooza. Si vizuri kuchota maji katika visima na kuingiza katika injini kwani maji hayo huwa na uchafu ambao hubaki kwenye rejeta na kuathiri utendaji kazi wake.

Rejeta huwa na mfuniko wake, mtumiaji wa chombo chochote chenye rejeta anapaswa kuhakikisha kuwa mfuniko uliopo ni mahsusi kwa rejeta hiyo, la sivyo kunaweza kutokea kuongezeka kwa joto la injini  kama ukitumia mfuniko tofauti.

Hakikisha sehemu ya mbele ya rejeta iko wazi na haina kipingamizi chochote kitakachozuia hewa kupita kwa urahisi ili iweze kufanya kazi kwa ufanisi.

Hakikisha rejea haivuji kwa namna yoyote ile, hii ni kuhakikisha kiwango cha maji hakipungui ndani ya mfumo wa upoozaji. Kama kuna sehemu inavuja, hakikisha fundi mwenye utaalamu anaziba haraka iwezekanavyo.