Mawaziri wa Ulinzi na viongozi wa ngazi ya juu wa nchi 27 za Kiarabu na Kiafrika jana Ijumaa walifikia makubaliano katika mkutano uliofanyika Sharam-Sheikh nchini Misri kuhusu kuimarisha ushirikiano baina yao katika vita dhidi ya ugaidi.
Kwa mujibu wa utangulizi wa azimio lililosomwa na Sedki Sobhi Waziri wa Ulinzi wa Misri mwishoni mwa mkutano huo, wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Sahel Sahara barani Afrika (CEN-SAD) wamekubaliana kuimarisha ushirikiano kwa lengo la kupambana na ugaidi na pia kuasisi kituo cha kuendesha mapambano dhidi ya ugaidi huko Cairo. Azimio hilo pia limetilia mkazo udharura wa kubadilishana taarifa na kufanya doria katika mipaka ya pamoja.
Mkutano huo wa siku mbili ambao ni wa tano wa Mawaziri wa Ulinzi wa Jumuiya ya Nchi za Sahel Sahara barani Afrika kuwahi kufanyika tangu kuasisiwa kwake mwaka 1998, ulimaliza kazi zake jana huku suala la ugaidi, harakati za makundi ya kigaidi na kuenea kwake hususan barani Afrika, limekuwa changamoto kubwa katika uga wa kimataifa.
Kuongezeka harakati na vitendo vya makundi ya kigaidi kama al Shabab, Boko Haram, al Murabitun, al Qaida katika nchi mbalimbali za bara la Afrika kama Nigeria, Niger, Mali, Somalia, Tunisia na baadhi ya nchi nyingine za bara hilo katika miaka kadhaa iliyopita, si tu kuwa kumesababisha kuuliwa na kujeruhiwa raia wengi wa nchi hizo bali pia kumezisababishia nchi hizo maafa ya kiuchumi yasiyoweza kufidika kutokana na kuvurugika hali ya usalama katika baadhi ya nchi hizo. Hii ni pamoja na kuwa aghlabu ya nchi hizo zinasumbuliwa na matatizo makubwa ya kiuchumi na ukosefu wa ajira.
Magendo ya silaha na dawa za kulevya ni masuala mengine yanayoyumbisha amani na utulivu katika nchi mbalimbali za bara la Afrika.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Sahel Sahara ambaye ni raia wa Nigeria ameashiria kwenye mkutano huo wa Sharam-Sheikh jinsi hali ya mambo katika nchi za Sahil Sahara inavyotia wasiwasi na kueleza kuwa silaha, dawa za kulevya na hujuma za makundi yenye kufurutu ada na ugaidi ni miongoni mwa mambo yanyotia wasiwasi mkubwa.
Weledi wa mambo wanasema kuwa, miongoni mwa sababu za kuongezeka harakati za makundi ya kigaidi barani Afrika ni kudodora ustawi wa kiuchumi na kisiasa katika nchi nyingi za bara hilo licha ya kuwa na maliasili na utajiri mkubwa.
Ripoti za taasisi za kimataifa zinaonesha kuwa, nchi nyingi za Kiafrika zinasumbuliwa na umaskini, ukosefu wa ajira na kukosekana uadilifu wa kijamii. Wakazi wengi wa nchi za bara la Afrika wanaishi chini ya mstari wa umaskini. Hii ni katika hali ambayo kukosekana uadilifu katika kugawa utajiri wa rasilimali na ufisadi wa baadhi ya watawala wa nchi hizo vimewawezesha magaidi kujipenyeza kwa urahisi katika baadhi ya nchi za Kiafrika na kuwashawishi vijana kujiunga na makund hayo kwa ahadi za kuboresha maisha yao.
Katika upande mwingineni, ustawi mdogo wa kisiasa pia umeandaa nyanja za kudhihiri na kueneza zaidi ugaidi barani Afrika. Katika nchi nyingi za bara hilo bado hakujachukuliwa hatua za maana za utawala wa demokrasia. Vita na mapigano ya kidini na kikabila yangali yanaendelea katika baadhi ya nchi za Kiafrika na baadhi ya viongozi wa nchi hizo wanaendelea kung'ang'amia madaraka kupitia ujanja wa kubadili katiba au kwa njia za kidikteta.
Pamoja na hayo yote, kuwepo madola ya Magharibi na ya kikoloni katika nchi hizo, ambayo yanayafadhili kwa silaha makundi ya kigaidi, kuchochea migogoro ya ndani na kuibua machafuko ili kutimiza malengo yao ya kikoloni, si tu kuwa kumepelekea kuenea makundi ya kigaidi barani Afrika, bali makundi hayo yameenea pia duniani kote kwa ujumla na suala hilo sasa limegeuka na kuwa hatari kwa ulimwengu mzima; hatari ambayo haitambui mipaka yoyote ile.
Leo hii weledi wa mambo wanasema kuwa, hakuna nchi inayoweza kuendesha vita dhidi ya ugaidi peke yake na kwa kujitegemea. Kwa msingi huo kuimarishwa ushirikiano wa kieneo na kimataifa katika nyanja mbalimbali za kijeshi, kiusalama na kiuchumi kunaweza kusaidia mikakati ya kuyaangamiza makundi ya kigaidi.
Mkutano wa Sharam-Sheikh nchini Misri na makubaliano yaliyofikiwa ni miongoni mwa hatua zilizochukuliwa katika kulipatia ufumbuzi suala la ugaidi.