Takwimu na ripoti zilizotolewa hivi karibuni kuhusu ukandamizaji wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya raia wa Palestina zinaonesha kutokea kwa maafa ya kutisha yaliyofanywa na Israel katika duru mpya ya ukatili wa utawala huo huko katika ardhi za Palestina katika miezi ya hivi karibuni.
Utawala wa Israel daima umekuwa ukiendeleza sera zake za kutaka kujitanua zaidi kwa kuzidisha ukandamizaji na kueneza hofu na woga, na suala hilo limewafanya walimwengui washuhudie maafa ya kutisha yanayofanywa na Israel huki Palestina.
Ripoti mbalimbali zinasema kuwa, Wapalestina wasiopungua 61 wameuawa tangu kuanza kwa mapambano ya Intifadha ya Quds. Taarifa iliyotolewa na Shirika la Haki za Binadamu Ulaya na Mediterranian inasema kuwa, Israel imewaua raia wasiopungua 61 wa Palestina katika vituo vya ukaguzi, na kambi za kijeshi ndani na nje ya miji ya Ukingo wa Magharibi na Quds tukufu tangu yalipoanza mapambano ya Intifadha ya Quds mwanzoni mwa mwezi Oktoba mwaka jana hadi hii leo. Shirika hilo limeongeza kuwa, kushadidi kwa mauaji yanayofanywa na jeshi la Israel dhidi ya Wapalestina kwa kisingizio eti wanawalenga Wazayuni, kunatia wasiwasi mkubwa. Shirika hilo la kutetea haki za binadamu limesema kuwa, watu hao waliouawa hawakuwa na hatari ya aina yoyote kwa askari wa Israel.
Taasisi hiyo ya Ulaya imesisitiza kuwa, viongozi na jeshi la Israel linakiuka na kukanyaga haki za binadamu na sheria za kimataifa. Vitendo hivyo vya Israel vinakiuka kifungu cha 27 cha Azimio la Geneva linalomlazimisha mvamizi kulinda maisha na mali za watu wa maeneo yanayokaliwa kwa mabavu.
Wakati huo huo Mratibu Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Mashariki ya Kati amelaani vikali kitendo cha askari mmoja wa Israel cha kummiminia risasi bila ya huruma kijana mmoja wa Palestina na kukitaja kuwa ni uovu mkubwa. Nikolay Mladenov amesema kuwa, umefika wakati wa kusitishwa ukatili na kuchukuliwa hatua chanya za kukomesha kukaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina na kurejesha amani na usalama.
Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, siku chache zilizopita kulirushwa mkanda wa video unaomuonesha askari mmoja wa Israel akimmiminia risasi kijana majeruhi wa Palestina katikati ya mji wa al Khalil na kumuua shahidi, suala ambalo limewakasirisha walimwengu.
Waziri wa Afya wa Palestina, Dakta Jawad Awadh, amesema askari wa Israel amefanya jinai ya kivita kwa kumpiga risasi kichwani na kumuua kijana huyo aliyekuwa amejeruhiwa na vilevile Mpalestina mwingine na kwamba ukatili huyo amenaswa na kamera.
Wakati huo huo Kamisheni ya Masuala ya Sheria ya Bunge la Israel imetangaza kuwa, imewasilisha muswada wa sheria ya kunyongwa Wapalestina wanaofanya operesheni dhidi ya Israel. Hii ni katika hali ambayo Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden, Margot Wallström, ametoa wito wa kufanyika uchunguzi kuhusu ukatili na mauaji yanayofanywa na Israel dhidi ya raia wa Palestina. Wito huo umewakasirisha sana viongozi wa utawala ghasibu. Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden ameashiria jinsi askari wa Israel wanavyowalenga kwa risasi hai Wapalestina wanaoandamana kwa amani na kuwazuia wafanyakazi wa huduma za afya kuwashughulikia majeruhi na kusema kuwa: "Kwa hakika Israel inawanyonga na kuwaua Wapalestina bila ya kuwafikisha mahakamani".
Kwa vyovyote vile kushadidi kwa ukatili na mauaji ya Israel dhidi ya Wapalestina katika miezi ya hivi karibuni kumezusha wimbi kubwa la upinzani wa jamii ya kimataifa.