Rais wa zamani wa Yemen amesema kuwa, Saudia inahusika katika machafuko yanayotokea kwenye nchi nyingi za Kiarabu.
Televisheni ya al Mayadeen imemnukuu Ali Abdullah Saleh akisema hayo leo katika hotuba yake ya kwanza kabisa mbele ya wananchi tangu baada ya Saudi Arabia kuanzisha mashambulizi yake ya kivamizi dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu. Ali Abdullah Saleh amehutubia wananchi mjini San'a na kusema kuwa, kuna wajibu wa kupigwa marukufu kuuziwa silaha utawala wa Aal Saud wa Saudi Arabia.
Rais huyo wa zamani wa Yemen amelilaumu Baraza la Usalama la umoja wa Mataifa kwa kushindwa kuchukua hatua za kivitendo za kukomesha jinai za Saudia dhidi ya wananchi wa Yemen na kulitaka baraza hilo litekeleze ipasavyo majukumu yake ya kuwalinda wananchi wa Yemen mbele ya jinai za ukoo wa Aal Saud.
Aidha amesema kuwa, anaunga mkono mazungumzo na utawala vamizi wa Saudia kama ambavyo amesisitizia pia wajibu wa wananchi wa Yemen kuwasaidia na kuwaunga mkono wale wote wanaopigania ukombozi wa nchi hiyo kama vile kundi la wananchi la Ansarullah.
Kabla ya hapo, rais huyo wa zamani wa Yemen alikuwa ametawaka wafuasi wake kuitumia tarehe 25 Machi, siku ulipoanza uvamizi wa Saudia nchini Yemen, kupaza sauti zao kulaani jinai za utawala huo wa kifalme.