Habari sanaa na michezo

Jumanne, 10 Machi 2026

T media news

Tanzania imeendelea kuimarisha nafasi yake kama kivutio cha kimataifa cha uwekezaji

 Tanzania imeendelea kuimarisha nafasi yake kama kivutio cha kimataifa cha uwekezaji kwenye sekta ya madini baada ya kuorodheshwa miongoni mwa maeneo yanayoongoza barani Afrika, kwa mujibu wa ripoti ya Fraser Institute, Annual Survey of Mining Companies 2025.


Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Tanzania imepata nafasi ya 34 kati ya maeneo 68 duniani yaliyotathminiwa katika Investment Attractiveness Index (IAI), kielezo kinachotumiwa na wawekezaji na kampuni za utafiti wa madini kuamua wapi waelekeze mitaji ya utafiti na maendeleo ya miradi.  

Katika muktadha wa Afrika, Tanzania imeendelea kushika nafasi ya juu kwa kuwa ya 4 barani Afrika katika IAI, ikifuata Botswana, Morocco na Zambia, hatua inayothibitisha ushindani wa Tanzania katika kuvutia mitaji ya kimataifa ya utafiti na uwekezaji wa madini.  


Ripoti inaonesha pia mwenendo chanya wa kupanda kwa alama za Tanzania, ambapo alama ya IAI imefikia 68.04 mwaka 2025, ikilinganishwa na 62.75 mwaka 2024 na 46.38 mwaka 2023 mwenendo unaoashiria kuongezeka kwa uaminifu na mvuto wa Tanzania kwa wawekezaji wa sekta ya madini.  

Kwa maelezo ya ripoti, IAI hujengwa kwa kuzingatia vipengele viwili vikuu vinavyoongoza maamuzi ya uwekezaji: uwezo wa kijiolojia wa rasilimali (mineral potential) na mazingira ya jumla ya kufanya biashara kwenye sekta husika. Ripoti hiyo inaeleza kuwa katika hesabu yake, asilimia 60 ya uzito huenda kwenye mineral potential na asilimia 40 huenda kwenye policy framework, ili kutoa taswira ya mvuto wa eneo husika kwa uwekezaji wa utafiti na uchimbaji.