Habari sanaa na michezo

Ijumaa, 6 Machi 2026

T media news

Takribani miaka mitano kabla ya kutumwa kwa Mtume Muhammad (s.a.w), Kaaba ilipata nyufa kubwa kutokana na mafuriko


 Takribani miaka mitano kabla ya kutumwa kwa Mtume Muhammad (s.a.w), Kaaba ilipata nyufa kubwa kutokana na mafuriko. Wakati huo haikuwa na paa, hivyo ilikuwa rahisi kuibiwa. Ndipo maquraysh wakakusanyika na kuamua kuijenga upya.


Mwanzoni waliogopa kuibomoa wakihofia huenda wakapatwa na jambo baya. Hatimaye mtu aitwaye Al-Walid ibn al-Mughira akawa wa kwanza kuanza kubomoa sehemu ya Kaaba. Walipomwona kuwa hakupatwa na madhara yoyote, wengine wakafuata na kuendelea kubomoa hadi wakafika kwenye msingi uliowekwa na Nabii Ibrahim (a.s).


Walikuta msingi huo ni imara sana, hivyo wakaacha kama ulivyo.


Walikubaliana pia kwamba katika ujenzi huo hawataweka mali yoyote haramu—isiwe mali ya riba, dhuluma wala dhambi. Lakini walipokusanya fedha, hazikutosha kujenga Kaaba juu ya misingi yote ya Ibrahim. Kwa hiyo wakalazimika kuacha sehemu ndogo nje ya jengo, ambayo leo inajulikana kama Hijr Ismail (au Al-Hatim). 


Pia waliweka paa na waliinua mlango wake juu ya ardhi ili waweze kudhibiti nani aingie ndani.


Walipofika mahali pa kuweka Black Stone, makabila yakagombana ni nani apate heshima ya kuliweka. Ugomvi huo ulikaribia kusababisha vita, na uliendelea kwa siku kadhaa.


Hatimaye wakakubaliana kwamba mtu wa kwanza kuingia kupitia mlango wa msikiti ndiye awe mwamuzi. Mtu wa kwanza kuingia alikuwa Muhammad (s.a.w). Walipomwona wakasema: “Huyu ni Al-Amin (mwaminifu), tunaridhia awe mwamuzi.”


Mtume (s.a.w) akawaamuru walete kitambaa. Akaweka jiwe jeusi katikati yake, kisha akaamuru kila kabila lishike upande wa kitambaa.


Wakalinyanyua wote pamoja hadi lilipofika mahali pake. Kisha Mtume (s.a.w) akalichukua kwa mkono wake mtukufu na kuliweka mahali pake.


Hivyo mgogoro ukaisha na wote wakaridhika.

Tukio hili limethibitishwa katika vitabu sahihi vya Seerah. Linaonyesha heshima aliyokuwa nayo Mtume Muhammad (s.a.w) miongoni mwa watu wake kabla ya kupewa Utume, pamoja na hekima yake, uadilifu na uwezo wake wa kutatua migogoro. Pia linaonyesha kuwa Allah alimwandaa tangu ujana wake ili awe mtu wa kuunganisha watu na kuzuia fitna.


Ukisoma kisa hiki, tafakari jinsi Allah alivyoyaunganisha nyoyo za watu kupitia yeye hata kabla ya wahyi kushuka. Alijulikana kwa ukweli na uaminifu wake.


Sambaza kisa hiki ili watu wajifunze sehemu ya historia yake tukufu, kwani kuonyesha watu kheri ni mlango mkubwa wa kupata malipo mema.


Kama umesoma kisa hiki mpaka mwisho basi usiondoke bure bali acha athari njema kwa kuandika moja miongoni mwa majina matukufu ya Allah Subhaanahu wataala ☝️ ♥️