
Afisa wa jeshi la Iran amesema kuwa jaribio lolote la Marekani au Israel la kutaka kuupindua utawala wa Iran kupitia "machafuko ya silaha" litakabiliwa na jibu la moja kwa moja ambalo linaweza kujumuisha kulenga kinu cha nyuklia cha Dimona cha Israel.
Afisa huyo aliongeza, katika matamshi yaliyobebwa na tovuti ya habari ya Iran, kwamba "kuanzisha mpango wowote unaolenga kuuangusha utawala kutailazimu Iran kulenga miundombinu ya nishati ya eneo hilo."
Ingawa Israel haijawahi kukiri rasmi kumiliki silaha za nyuklia, tathmini nyingi za kimataifa zinaonyesha kuwa inamiliki silaha hizo. Mpango wake wa nyuklia unachukuliwa kuwa moja ya silaha za siri zaidi za maangamizi makubwa duniani.
Israel haijatia saini Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia, mkataba wa kimataifa unaolenga kuzuia kuenea kwa aina hii ya silaha.
Kwa sababu hii, vifaa vyake vya nyuklia haviko chini ya mfumo wa ulinzi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, ambayo inaruhusu wakala kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa vifaa vya nyuklia katika nchi ambazo zimejiunga na mkataba.
Uwezo wa nyuklia wa Israeli umebakia kuwa mada ya makadirio ya kijasusi yasiyo na uhakika tangu miaka ya 1960, ilipoanza kuendesha kinu cha nyuklia cha Dimona kwenye jangwa la Negev.
Katikati ya miaka ya 1980, sehemu ya uwezo huo ilifichuliwa baada ya fundi wa zamani wa kinu Mordechai Vanunu kupatia gazeti la Uingereza maelezo na picha za kile alichosema ni vichwa vya nyuklia vya Israel.
Habari iliyofichuliwa na Vanunu ilisababisha kutathminiwa upya kwa makadirio ya hapo awali ya ukubwa wa ghala la nyuklia la Israel, ambalo mwaka 2003 lilikadiriwa kuwa si chini ya vichwa 100 vya nyuklia na ikiwezekana 200.