Katika siku ya saba ya vita vya kukabiliana na uchokozi wa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel,
Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu limetangaza wimbi la ishirini na moja la Operesheni “Ahadi ya Kweli 4”, likihusisha mashambulizi ya pamoja ya makombora na ndege zisizo na rubani (droni), pamoja na kurushwa kwa makombora ya Kheibar yenye vichwa vingi vya kivita dhidi ya malengo yaliyoko katikati ya Tel Aviv.
Kwa mujibu wa mwandishi wa Pars Today, Shirika la Habari la Mehr limeripoti kuwa, siku ya saba ya vita imeenendelea huku uwanja wa mapambano ukishuhudia kuongezeka kwa kiwango cha mashambulizi ya kulipiza kisasi kutoka Iran.
Operesheni “Ahadi ya Kweli 4” imeendelea kwa mawimbi mfululizo, ikitumia makombora ya kisasa ya Kheibar kulenga vituo nyeti ndani ya Tel Aviv. Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu pia limetangaza utayari wake kamili wa kuendeleza mapambano ya muda mrefu na kuanzisha matumizi ya mifumo mipya ya silaha.
Wakati huohuo, taarifa zinasema makombora ya Iran yameweza kuharibi mfumo wa Marekani wa ulinzi wa anga wa THAAD nchini Jordan.
Siku ya Ijumaa asubuhi, katika taarifa namba 22 ya Operesheni “Ahadi ya Kweli 4”, kitengo cha uhusiano wa umma cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kilitangaza kwamba: “Wimbi la ishirini na mbili la Operesheni “Ahadi ya Kweli 4” lilianzishwa kwa kaulimbiu tukufu “Ya Hussein bin Ali (amani iwe juu yake)”, likihusisha kurushwa kwa makombora ya Kheibar, Khorramshahr‑4, na Fattah. Mashambulizi hayo yalielekezwa dhidi ya malengo ya Marekani na utawala wa Kizayuni kuanzia Ghuba ya Uajemi hadi Tel Aviv, kama hatua ya kulipiza kisasi dhidi ya walioua watoto wa Iran katika tukio la shule ya Minab.
Katika wimbi hili lenye nguvu, kufuatia tangazo la Walinzi wa Mapinduzi kuhusu kuongeza na kupanua mashambulizi, pamoja na makombora makubwa ya balistiki, pia kulitumika kombora zito sana la “Khorramshahr‑4” lenye kichwa cha kivita cha tani mbili na kasi inayofikia takribani Mach 14, ambalo lilielekezwa dhidi ya malengo ya maadui wanaoihasimu taifa la Iran.
