Jeshi la Marekani kupitia makao makuu yake ya kijeshi Pentagon linajiandaa kuomba mabilioni ya dola zaidi kutoka Bunge la Marekani ili kuendelea kufadhili operesheni za vita dhidi ya Iran.
Ripoti zinaonyesha kuwa katika saa 48 za kwanza za mapigano, majeshi ya Marekani yalitumia silaha na mabomu yenye thamani ya dola bilioni 5.6 katika mashambulizi dhidi ya Iran
Taarifa hiyo imewasilishwa kwa wabunge wa Marekani na imeibua mjadala kuhusu gharama kubwa ya vita na matumizi ya haraka ya silaha za kisasa za Marekani
Ikulu ya Marekani inatarajiwa kuwasilisha ombi la bajeti ya ziada ya ulinzi lenye thamani ya makumi ya mabilioni ya dola ili kuendelea na operesheni za kijeshi katika vita hivyo.
Jeshi la Marekani kupitia Pentagon limeanza kutumia sehemu ya akiba yake ya makombora ya ulinzi wa anga aina ya Patriot katika maeneo ya Bahari ya Hindi na Pasifiki, hatua inayohusishwa na ongezeko la mvutano wa kijeshi duniani, hususan vita vinavyoihusisha Iran.
Taarifa za kijeshi zinaonyesha kuwa Marekani imekuwa ikitumia makombora ya Patriot na mifumo mingine ya ulinzi kukabiliana na makombora na droni zinazotoka kwa Iran au washirika wake katika eneo la Mashariki ya Kati.
Hata hivyo, wataalamu wa ulinzi wanaonya kuwa matumizi makubwa ya makombora haya yanaweza kupunguza akiba ya Marekani, jambo ambalo linaweza kuathiri uwezo wa kijeshi wa nchi hiyo katika maeneo mengine muhimu kama Indo-Pacific, ambako Marekani pia inajiandaa kukabiliana na vitisho vya kijeshi kutoka China.
Aidha, ripoti zinaonyesha kuwa baadhi ya mifumo ya ulinzi wa makombora, ikiwemo Patriot na THAAD, imehamishwa kutoka maeneo kama Korea Kusini kwenda Mashariki ya Kati ili kusaidia operesheni dhidi ya Iran.

