Wamebutuliwa! Ndiyo msemo unaoweza kuusema baada ya Mzee Abdul, ambaye ni baba mkwe wa wanawake wawili, Zarinah Hassan ‘Zari The Bossy Lady’ na Mwanamitindo Hamisa Mobeto ambao waliumaliza mwaka jana kwa kuchafuana mitandaoni, mmoja akimuita mwenzake mchawi na mwingine akidaiwa kuwa ni changudoa mzee, jambo ambalo mzee huyo hakupendezwa nalo.
Akizungumza na Amani juzikati, Mzee Abdul alisema anachukizwa na kitendo cha wanawake hao ambao wote wamezaa na mwanaye, kuvuana nguo mitandaoni wakati kila mmoja ana haki sawa.
Mwanamitindo Hamisa Mobeto.
MSIKIE MZEE ABDUL
“Ninawasihi hawa wanawake waache malumbano katika mitandao ya kijamii, kwa sababu kila mmoja amezaa hivyo wote wana nafasi na haki sawa kwa vile hakuna aliyeolewa hadi sasa.
“Maneno wanayotoleana mitandaoni ni mabaya na yananichukiza mno, sasa naomba niwaase vijana wangu waache mara moja kwani wote wana haki sawa, mwanangu bado hajaoa na huenda mmoja wao akaolewa lakini na mwingine akapewa heshima yake kama mzazi, lakini pia bado wote wawili wanaweza kuolewa kwa vile imani ya dini ya mwanangu inaruhusu.”
AWATAKA KUNYAMAZA
Mzee huyo alienda mbali zaidi na kuwasihi Zari, aliyezaa watoto wawili na Hamisa mwenye mtoto mmoja, wanyamaze wakati kila mtu akisubiri uamuzi wa kijana wake.
“Kitu ambacho nina uhakika nacho ni kuwa kila mmoja kwa kitendo cha kuzaa na mwanangu, ataambulia chochote kitu kwani wana haki.
Zarinah Hassan ‘Zari The Bossy Lady’ .
“Unajua wasichokijua ni kuanika siri zao mitandaoni wanajiabisha na kutukanana vile wanajiabisha, kwetu sisi wazazi tunaonekana hatuna busara kuendelea kunyamazia ugomvi huo, mimi ninachoweza kusema ni kuwaomba wanyamaze, kila mmoja afanye mambo yake, atakayeendelea kulumbana na mwenzake ndiye ataonekana ana matatizo, lakini atakayekaa kimya, huyo ndiye atakuwa mwanamke wa kuoa,” alisema.
AMTAKA MAMA ESMA KUWA NA BUSARA
Mzee Abdul aliamua kumchana mzazi mwenzake, Mama Esma kwa kumtaka kuwa na busara kwa vile anaonekana kuchagua upande mmoja ambao anauunga mkono kupitia mitandao, kitu alichodai siyo sahihi.
“Namwambia mama Esma awe na busara, yeye ni mzazi, tabia yake ya kuchagua upande na kuendeleza vijembe siyo nzuri kwani anajua wazi kuwa mtoto wa Mobeto pia ni wetu, siyo vizuri, yeye kama mzazi angewashauri nina uhakika wangemsikiliza lakini nashangaa amechagua upande mmoja wa Zari,” alisema Mzee Abdul.
TUJIKUMBUSHE
Mwishoni mwa mwaka jana, Zari na Mobeto walirushiana vijembe vikali kwenye mitandao ya kijamii kila mmoja akimponda mwenzake. Wakati Zari akidai Mobeto hana hadhi ya kushindana naye, mwenzake huyo alimponda kuwa ni changudoa mzee, kitu kilichomchafua zaidi mama huyo wa watoto watano.
Kufuatia madai hayo, Zari alirusha kombora kwa kumuita mwenzake mchawi, akidai ‘ndumba’ zake alizotumia kumuibia mpenzi wake zimeisha nguvu na akijinadi kuwa yeye ni changudoa mzee mwenye mafanikio.
Kabla ya hapo, wawili hao walifanya shoo siku moja nchini Uganda katika maeneo yaliyo jirani, kitu ambacho kilionesha dhahiri kuwa bado wana bifu.
Chanzo: Global Publishers