Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imelazimisha sare ugenini dhidi ya Benin kwenye mchezo wa kirafiki wa kalenda ya FIFA uliomalizika jioni hii.
Tanzania ambayo imecheza bila ya nahodha wake Mbwana Samatta ambaye ni majeruhi, ilijikuta ikilazimika kusubiri hadi kipindi cha pili ili kusawazisha bao la Benin lililofungwa na Stephan Sessegnon dakika ya 30.
Baada ya kurejea kutoka mapumziko Taifa Stars ilirudi na nguvu mpya ambapo walifanya mashambulizi kadhaa kupitia kwa washambuliaji wake Simon Msuva, Shiza Kichuya na Elias Maguli.
Jitihada binafsi za Shiza Kichuya zilizaa matunda dakika ya 51 baada ya kuwapita walinzi akitokea pembeni kushoto, kisha kupiga krosi ambayo ilitendewa haki na Elias Maguli kwa kuiandikia Taifa Stars bao la kusawazisha.
Baada ya bao hilo timu zote ziliendelea kushambuliana lakini hakuna timu ambayo iliona lango la mwenzake hadi mwamuzi alipomaliza mchezo huo matokeo yakabaki kuwa sare ya 1-1.