Wakati utata ukizidi kugubika kushikiliwa, maisha na mwenendo wa Dk Louis Shika anayetuhumiwa kuvuruga mnada wa nyumba za bilionea Said Lugumi, imebainika kuwa ndugu zake walishamtenga baada ya kutoweka kijijini na kutojihusisha na familia.
Dk Shika alipata umaarufu kwa muda mfupi baada ya kushiriki katika mnada wa nyumba tatu za kifahari jijini Dar es Salaam na kuibuka mshindi, akiwa ameweka dau la takriban Sh2 bilioni, lakini akashindwa kufanya malipo ya awali ya asilimia 25.
Umaarufu wake ulitokana na hali ya kujiamini aliyoonyesha wakati akipandisha bei ya nyumba hizo na wakati fulani, akitaja bei ya juu kwa kusema kuwa ndiyo “900 ingependeza”, lakini akashindwa kufanya malipo kama ilivyotakiwa, hali iliyomfanya aanze kufuatiliwa na vyombo vya dola na baadaye vyombo vya habari.
Kutokuwa na fedha kulingana na mahitaji ya mnada huo, makazi, maisha na maelezo yake yalishangaza wengi waliofuatilia maisha yake.
Na waandishi wa habari wa Mwananchi waliofika kijijini kwao mkoani Mwanza, walikuta hadithi mpya.
Mwananchi ilipokutana na kaka mkubwa wa Dk Shika anayeitwa Pelanya Lunyalula mwenye umri wa miaka 84, ilimkabidhi gazeti lenye picha ya “bilionea’ huyo. Alipoiona alibubujika machozi akisema ni mdogo wake anayeitwa Shika.
“Kwetu wana ukoo, Shika tunamhesabu kwenye kundi la ndugu wasiokuwepo (tumetumia neno letu kuepusha makali), maana hajawahi kurejea nyumbani licha ya baba, mama na ndugu wengine kufariki na yeye kupata taarifa,” alisema Lunyalula akiwa nyumbani kwake kitongoji cha Misheni, Kijiji cha Chamugasa jana.
“Uamuzi wa kumtenga Shika ulifikiwa katika kikao cha wana ndugu wakati wa msiba wa baba yetu mkubwa, Mzee Kisula Buselele. Hilo lililomfika atalimaliza mwenyewe kama alivyolianzisha kwa sababu hatumhesabu kama ndugu.”
Lunyalula, baba wa watoto tisa anasema mara ya mwisho alionana na Dk Shika wakati akiwa kijana na wakati huo mdogo wake alikuwa hajaenda masomoni nchini Urusi.
“Sikumbuki mwaka. Ila ni miaka ile ya operesheni ya wahujumu uchumi (miaka ya themanini mwanzoni). Tangu wakati huo hajarudi nyumbani wala kuwa na mawasiliano na familia,” alisema Lunyalula ambaye ni mtoto wa pili kuzaliwa kwenye familia ya Mzee Lunyalula Kidola na Mama Wile Ngongo.
“Kwa kipindi chote hicho, huwa tunasikia tu kuwa amerudi likizo kutoka Ulaya, lakini anaishia Dar es Salaam na kurudi bila kufika nyumbani,” alisema Lunyalula ambaye anafuatiwa na wadogo watatu kabla ya Dk Shika. Aliwataja waliomtangulia Dk Shika kuwa ni Dk Jeremiah, Mpelwa na mwingine anayesema alifariki kabla ya kupewa jina.
“Kama unavyoiona hii nyumba inakaribia kuanguka. Hii kweli inaweza kuwa nyumbani kwao mtu anayejiita daktari bingwa aliyesoma Ulaya? Hailingani, na hata wenzake wakija kuona picha ya nyumbani kwao, watashangaa,” alisema.
Nyumba ya familia hiyo ya matofali ya udongo na kuezekwa kwa mabati, ilijengwa na Dk Shika na ndugu yake Jeremiah aliyefariki Desemba 19, 1992 kwa mujibu wa maandishi kwenye kaburi lake lililo pembeni mwa makaburi ya wazazi wake.
Kwa mujibu wa Lunyalula, Dk Jeremiah aliyewahi kufanya kazi hospitali za Bugando ya Mwanza na KCMC mjini Moshi, ndiye alikuwa wa kwanza kwenda kusoma Urusi na kufuatiwa na Dk Shika.
Mwenyekiti wa Kitongoji
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Emmanuel Wakenya alieleza kushangaa taarifa kwamba Dk Shika ni mmoja wa watu kutoka eneo hilo.
“Tumeshtuka kujua kumbe mtu anayeitwa Dk Louis Shika ni ndugu yetu hapa kijijini aliyepotea muda mrefu tangu tukiwa watoto na hajarejea hadi leo,” alisema.
Wakenya, ambaye ni mpwa wa Dk Shika, alisema alimfahamu ‘bilionea’ huyo akiwa mtoto, lakini hajawahi kumwona wala kupata taarifa zake.
Mwenyekiti huyo aliyeishukuru Mwananchi kwa kuwapelekea nakala ya gazeti lenye habari na picha ya Dk Shika, alisema licha ya kutorudi nyumbani, ‘daktari’ huyo hajawahi kuoa wala kupeleka mke au watoto kijijini hapo.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Lunyalula.
“Mimi sina mke kwa sasa, lakini nimewahi kuoa na kuzaa watoto tisa kabla ya kutengana na mke wangu mwaka 2004. Shika yeye hatujui habari zake kuhusu ndoa na familia,” alisema Lunyalula.
Ndugu wengine wa Dk Shika, kwa mujibu wa kaka yake Lunyalula ni dada yao mkubwa Cecilia, Jeremiah (marehemu), Mpelwa, Pius, Kefline, Hellen, Dotto na Paulo.
Jirani hamfahamu Dk Shika
Jirani wa familia ya Dk Shika kijijini, Ng’washi Kabukabu hamjui mtu mwenye jina hilo.
“Mimi huyo Shika simfahamu wala sijawahi kumsikia hadi leo mnaponiuliza habari zake. Ila familia hii ni kati ya majirani tunaoishi nao vizuri,” alisema mama huyo.
Makazi yalivyo
Jijini Dar es Salaam, jirani zake eneo la Tabata Mawezi, takriban mita 700 kutoka kituo cha daladala cha Tabata Mawenzi, walikuwa na hadithi nyingine zinazoendelea za kusisimua.
“Unajua mambo mengine yanashangaza. Mtu anapozeeka akili zinarudi kama za mtoto na huyu ni babu ujue. Hata suala la umeme au maji hapa huwa halipi atatoa wapi hela?” alisema mama mmoja mpangaji mwenzake aliyeomba jina lake lisitajwe.
Mama huyo aliwaonyesha waandishi wa gazeti hili chumba ambacho anaishi Dk Shika.
Kwa kutokea dirishani ambako hakuna pazia, unaweza kubaini kuwa aliondoka mapema siku ya mwisho, mithili ya mtu aliyekuwa anawahi sehemu; kitanda cha ukubwa mita 4x6 kikiwa hakijatandikwa, juu yake kukiwa na magazeti, karatasi, nguo na vitabu na chandarua hakijashushwa vizuri.
Pembeni kuna kabati likiwa na mabegi mawili ya nguo, kuna mabeseni matatu madogo, dumu moja la maji, kikaango cha mayai au chapati, kikombe kimoja cha plastiki na jiko la mafuta ya taa.
Pembeni kuna vitanda na chaga zimeegeshwa nusu ya chumba chote, kandambili, nguo baadhi zimetundikwa na mifuko myeusi.
“Hivyo vitanda ni vya baba mwenye nyumba na wakati akija alivikuta. Si unajua babu hana vitu vingi kama ulivyoona, ndiyo maana anatumia vivyo hivyo,” alisema jirani mmoja.
‘Bilionea’ ni mtu wa kawaida
Mmoja wa kina mama wanaouza chakula eneo la jirani na ambaye alijitambulisha kwa jina la Mama Glory alisema Dk Shika “ni mtu wa kawaida sana”.
“Huwa anakuja hapa kunywa chai ingawa anapenda maharage na chapati mbili au moja,” alisema.
“Nilikuwa namjua kama babu, hilo la dokta ndiyo nimelijua sasa. Babu akija hapa hana tatizo, atakula na akimaliza ataondoka. Si msumbufu kabisa ni mtu wa kawaida kabisa.”
Kauli ya Mama Glory inafanana na ya mama lishe mwenzake aliyejitambulisha kwa jina moja la Rose.
“Kumbe babu ana hilo jina! Nilivyosikia nilishangaa ila huwezi kumjua mtu kama ana hela kwa kumuangalia,” alisema.
“Ni mteja wetu hapa na anapenda kula ugali, ila nilishtuka nilivyoona katika mitandao na baadaye kwenye taarifa ya habari usiku. Huwezi kumjua mtu kama ana hela kwa kumuangalia, labda ni kweli.”
Mmoja wa watoa huduma za kifedha kwa simu za mikononi ambaye hakutaka kutaja jina kwa kuhofia kutafutwa kutoa ushahidi, alisema huwa anamuona mtaani ‘bilionea’ huyo.
“Mara nyingine huwa anakuja kutoa hela katika simu na nilishangaa nilipoona katika mitandao kwamba kanunua majumba ya Lugumi kwa kuwa huwa akija kutoa hela, haizidi Sh5,000,” alisema.
“Utakuta anatoa Sh4,500, Sh3,500 na wakati mwingine anatoa Sh2,500. Kutokana na chenji kusumbua huwa namkwepa.”
Asaidiwe, asiwekwe ndani
Hashim Said, anayeuza duka karibu na eneo hilo, alisema tangu alipomfahamu miezi minne iliyopita hakuwahi kununua kitu chochote dukani kwake.
“Hapa anaweza akaja na akakuulizia kitu ambacho hakipo na ukikileta hanunui. Hiyo ndiyo ilikuwa kawaida yake,” alisema na kuongeza kuwa huwa anawadokezea kuwa alikuwa akienda Urusi.
“Inavyoonekana mwanzoni alikuwa vizuri kiuchumi japo nasikia anapokaa kawekwa tu. Kwa mazingira yake mwenyewe na maisha anavyoishi hapa mtaani, sijui kama anaweza kuwa na fedha. Wewe mtu kama anapitisha siku mbili bila kula atakuwa na hela?” alihoji Said.
“Ninachokiona huyu mzee hapaswi hata kuwekwa ndani. Ukifuatilia hata mazungumzo yake kuna vitu kama viliwahi kumtokea kwani katika mazungumzo yetu hapa aliwahi kusema alifungwa ila ukimuuliza wapi hasemi. Huyu anapaswa kusaidiwa na si kuwekwa ndani.
“Kwa hiyo anapaswa kutafutiwa wataalamu wa saikolojia wakazungumza naye na si kumuweka ndani au kumpeleka mahakamani. Ujue hana wasiwasi kabisa kwani juzi alipokuja na polisi hapa kama wanne alikuwa akitembea kwa kujiamini kabisa.”
Habari hii imetayarishwa na Peter Saramba,Ngollo John na Ibrahim Yamola