SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 15 Novemba 2017

T media news

Rais Magufuli aagiza Makao Makuu ya TANESCO kubomolewa

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 15 Novemba 2017, amerejea jijini Dar es salaam akitokea kijijini kwake Chato, mkoani Geita.

Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dare es salaam, Mhe. Rais amepokelewa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda na viongozi wengine wa mkoa.

Baada ya kutoka Uwanja wa Ndege, Rais Magufuli akiwa ameongozana na Makamu wa Rais pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, amekagua Ujenzi wa Daraja la juu Tazara ( Tazara Fly-Over) na Ujenzi wa Daraja la ghorofa tatu la Ubungo ( Ubungo Interchange)

Akikagua maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Ubungo, Rais Magufuli amemuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara nchini TANROADS  Mkoa wa Dar es salaam Mhandisi Ndyamukama Julius kuvunja sehemu ya jengo la TANESCO na jengo la Wizara ya Maji yaliyopo katika eneo la hifadhi ya barabara ili kupisha ujenzi wa miundombinu ya daraja hilo.

”Sheria ya hifadhi ya barabara katika eneo hilo ni mita tisini kila upande kutoka katikati ya barabara hivyo ni lazima sheria hiyo iheshimiwe ili kuharakisha ujenzi wa Daraja la ghorofa tatu katika eneo hilo la Ubungo uanafanyika bila vikwazo kwani sheria ni msumeno haina budi kuzingatiwa hata na Serikali yenyewe” amesema Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli ameiagiza TANROADS kutangaza tenda ya ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita kumi na sita (16) kutoka eneo linapoishia Daraja la ghorofa tatu katika eneo la Ubungo kuelekea Chalinze ili itanuliwe kwa lengo la kurahisha usafiri katika jiji la Dar es salaam.

Rais Magufuli amewataka Makandarasi wanaojenga Daraja la Tazara na Ubungo kuharakisha ujenzi wa madaraja hayo usiku na mchana ili yaweze kumalizika kwa wakati ama kabla ya muda huo katika kurahisisha maendeleo ya kibiashara katika jiji la Dar es salaam.

”Dar es salaam ni jiji la kibiashara hivyo hakuna budi miundombinu yake ya usafiri iweze kurahisha usafirishaji wa bidhaa mbalimbali kutoka ndani ya jiji na nje ya jiji la Dar es salaam” amesema Rais Magufuli.

Mhandisi wa Masuala ya Usalama wa Ujenzi Mhandisi Richard Baruani amemueleza Rais Magufuli kuwa Ujenzi wa Daraja la Tazara umefikia asilimia 64 ambapo Daraja hilo linatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba 2018.

Kwa upande wa Daraja la ghorofa tatu la Ubungo, Mhandisi Mshauri Reginald Kayanga amesema  ujenzi wake unatarajiwa kuanza rasmi Desemba 2017.

Jaffar Haniu

Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

15 Novemba, 2017