Aliyekuwa Mhasibu mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Godfrey John Gugai amejisalimisha katika taasisi hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Kamishna Valentino Mlowola amesema Gugai amejisalimisha na hatua za kisheria zinaendelea.
"Ni kweli amejisalimisha na yupo chini ya vyombo vya ulinzi na usalama na hatua zaidi za kisheria zitafuata" amesema Kamishna Mlowola
Mtumishi huyo anatuhumiwa kujipatia mali kinyume cha Sheria za Utumishi wa umma huku Takukuru wakidai kwamba kama atadhibitisha uhalali wa umiliki wake ataachiwa na akishindwa atachukuliwa hatua.
Gugai amejisalimisha ikiwa ni siku moja imepita tangu Takukuru ilipotangaza zawadi ya Sh 10 milioni kwa mwananchi yoyote ambaye angefanikisha kumtia nguvuni mtumishi huyo.
Hata hivyo, Kamishna Molowa ameshindwa kufafanua kama amejisalimisha mwenyewe au kuna mtu katoa taarifa.