Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza orodha nyingine yenye wanafunzi 1,775 wa Mwaka wa Kwanza waliofanikiwa kupata mikopo na hivyo kufanya jumla ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliopangiwa mikopo hadi sasa kufikia 31,353.
Katika Awamu ya Kwanza, wanafunzi 10,196 wa mwaka wa kwanza walipangiwa mikopo, Awamu ya Pili (11,481), Awamu ya Tatu (7,901).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana (Jumapili, Novemba 12, 2017) na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq Badru, orodha kamili ya wanafunzi hao inapatikana katika tovuti ya Bodi (www.heslb.go.tz) na pia imetumwa kwa vyuo husika jana ili kuwawezesha wanafunzi kufanya usajili na kuendelea na masomo.
“Tumekua tukifanyia kazi orodha za udahili ambazo tumekuwa tukipokea, na kila tunapokamilisha, tunatoa orodha za wanafunzi waliopangiwa mikopo ambao wana sifa – leo tumetoa hao 1,775,” alisema Bw. Badru.
Bw. Badru, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari pia alikumbusha kuwa kiasi cha shilingi 427.54 bilioni zimetengwa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi kwa mwaka 2017/2018 na tayari Serikali imeshatoa shilingi 147.06 bilioni kwa ajili ya robo ya kwanza ya mwaka huu wa 2017/2018.
Fedha hizo, shilingi 427.54, ni kwa ajili ya jumla ya wanafunzi 122,623 wa mwaka wa kwanza na wale wanaoendelea na masomo.
Wakati huohuo, HESLB imetangaza kufungua dirisha la rufaa kuanzia kesho, Jumatatu, Novemba 13, 2017 hadi Novemba 19, 2017 ili kuwapa fursa waombaji wote ambao hawajaridhika na upangaji wa mikopo kuwasilisha rufaa kupitia vyuo walivyopata udahili.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji huyo wa HESLB, lengo la HESLB ni kuhakikisha wanatangaza orodha ya majina ya waombaji mikopo waliofanikiwa katika rufaa zao ifikapo au kabla ya tarehe 30 Novemba mwaka huu.
“Tunatoa wito kwa uongozi wa vyuo vyote kupokea maombi ya rufaa za wanafuzi na kuwasilisha kwa Bodi ya Mikopo kabla ya Novemba 22, 2017 ili kuiwezesha Bodi kutoa orodha ya waombaji waliofanikiwa katika rufaa zao ifikapo Novemba 30, 2017,” alisema Bw. Badru katika taarifa yake.
Maelezo ya kina kuhusu utaratibu wa kuwasilisha rufaa yatatolewa kupitia tovuti ya Bodi (www.heslb.go.tz).