SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 13 Septemba 2017

T media news

Zitto kupigwa marufuku kuzungumza bungeni

Kwa mara nyingine tena Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai (Mb) amemuagiza Zitto Kabwe kufika mbele ya Kamati ya Maadili ya Bunge kuhojiwa kutokana na kuendelea kuudhalilisha mhimili wa Bunge.

Spika Ndugai ametoa agizo hilo leo katika kikao cha Bunge vinavyoendelea mjini Dodoma ambapo amesema, Zitto Kabwe ambaye ni Mbunge wa Kigoma Mjini ameendelea kudhalilisha mhimili huo licha ya kuwa ameonywa na kutakiwa kufika mbele ya kamati kujieleza sababu za kufanya hivyo.

Akizungumza baada ya kipindi cha maswali na majibu, Ndugai amesema kuwa anaweza kumzuia Zitto asiongee bungeni katika kipindi chote cha ubunge na kwamba hatakuwa na kitu cha kumfanya.

“Zitto utapambana na spika kweli! Naweza kukupiga marufuku kuongea humu mpaka miaka yako yote ikaisha na hakuna pakwenda. Hakuna cha swali, hakuna cha nyongeza, hakuna cha kuongea chochote humu ndani ya Bunge. Utanifanya nini?”

Aidha Spika Ndugai amemtaka Mbunge Zitto Kabwe kupambana na kitu kingine lakini sio yeye.

Awali jana Zitto alitakiwa kufika mbele ya kamati kuhojiwa baada ya kusema kuwa mhimili wa bunge umewekwa mfukoni na mhimili fulani wa serikali.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter jana, Zitto aliendelea kuandika habari zilizokosoa namna Spika Ndugai anavyouongoza mhimili huo huku akisema kwamba hajafika hata asilimia 10 ya Annie Makinda.

“Kwa haya ya Spika sina sababu nayo, lakini ya kulidharau Bunge hayo sitaweza kuyavumilia nitalinda mhimili huu kwa nguvu zangu zote,” amesema Ndugai.

Nguai amesema kuwa, kama atawaacha wabunge waudharau mhimili huo, atashindwa kuwashughulikia wananchi huko nje ambao wataudharau mhimili huo.