SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumanne, 5 Septemba 2017

T media news

Breaking: Watoto waliotekwa Arusha wakutwa wamefariki

Wakati harakati za kendelea kuwatafuta watoto wawili kati ya wanne waliokuwa wametekwa jijini Arusha zikiendelea, taarifa za kusikitisha na mamlaka husika leo jioni zimeeleza kuwa, watoto hao wawili wamekutwa wakiwa wamefariki katika shimo la choo ambalo bado halikuwa limeanza kutumika.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Olkerian huko Olasiti jijini Arusha, Daudi Safari amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ingawa kumekuwa na mkanganyiko kuhusu eneo walipokuwa watoto hao kama ni shimo jipya la choo au kisima.

Miili ya watoto iliyookotwa ni ya Moureen David na Ikram Salum ambapo wenzao wawili Ayoub Fred na Bakari Seleman tayari walikuwa wamepatikana kutoka kwa watekaji hao waliokuwa wakidai kutumiwa fedha.

Septemba 2 mwaka huu, Samson Petro (18) alikamatwa na Jeshi la Polisi Mkoani Geita akituhumiwa kuhusika katika utekaji wa watoto mkoani Geita na Arusha.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo alithibitisha kukamatwa kwa kijana hiyo ambapo alisema alikamatwa katika nyumba ya kulala wageni ya Shitungului iliyopo Mji Mdogo wa Katoro akiwa na mtoto mdogo mwenye miaka miwili.

Aidha, Polisi jijini Arusha walimhoji kaka yake na Petro ambaye ni Askari wa FFU kwa tuhuma za kuhusika na utekaji huo.