Na Tiganya Vincent-Tabora
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ameagiza kukamatwa kwa wazazi wenye tamaa ya fedha ambao wamekuwa wakiwakatisha masomo mabinti zao kwa ajili ya kuwaozesha.
Mhe. Majaliwa alitoa kauli hiyo jana Wilayani Uyui katika mkutano wa hadhara
Alisema kuwa kuanzia sasa Watendaji wanatakiwa kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya dola bila woga wazazi wa binti na wale wa kijana wanaokatisha masomo ya watoto wa kike kwa lengo la kuwaozesha.
Waziri Mkuu alisema kuwa Serikali haitawavulia wazazi na watu wanaochangia kurudisha maendeleo ya wasichana kwa kisingizio cha kuwafungisha ndoa wakati bado ni wanafunzi.
“Nawaagiza Watendaji wote kuwakamata wazazi wa binti na wale kijana ambao mtawakuta wakiwa wanawaozesha mabinti wao ambao kimsingi walipaswa kuwa shule……msimuogope mtu wakamateni wote wawe wazazi wa binti hata wa yule anayetarajia kuoa ili hatua kali za kisheria dhidi yao ziweze kuchukuliwa” alisisitiza Mhe. Majaliwa.
Aliwaonya pia vijana ambao wanamiliki na kuendesha pikipiki maarufu kama boda boda ambao wamekuwa wakiwapakia wanafunzi kwa lengo la kuwarubuni ili wajihusishe na vitendo vya ngono kuacha mara moja.
Waziri Mkuu alisema mtu atakayekamatwa Serikali itamfikisha Mahakamani ili aweze kupata adhabu kali.
Alisisitiza kuwa ni vema wakaacha wanafunzi hao wakasoma na sio kuwarubuni.
Mkoa wa Tabora ni miongoni mwa mikoa mitatu hapa nchini inayoongoza kwa mimba na ndoa za utotoni.