Na: Genofeva Matemu – WHUSM
Uongozi mpya wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) umetakiwa kufikia Januari mwakani kuwajibika kama mashirika mengine ya mpira wa miguu duniani yanavyowajibika kuchapisha taarifa ya mapato na matumizi kwenye magazeti ili wananchi wapate fursa ya kufahamu namna fedha zinavyopatikana na jinsi zinavyotumika katika kuboresha na kuendeleza usimamizi bora wa soka nchini.
Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe wakati wa kufunga Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) jana katika ukumbi wa St. Gasper Mkoani Dodoma
Aidha Mhe. Mwakyembe aliwapongeza viongozi wapya waliochaguliwa kuiongoza TFF kwa muda wa miaka minne kwa kuwataka kufanya kazi kwa ushirikiano na kwa pamoja katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku huku akiwapongeza washiriki wote waliothubutu kuwania uongozi katika nafasi mbalimbali wakati wa uchaguzi Mkuu wa TFF wa mwaka huu.
Kwa upande wake Rais mpya wa TFF Bw. Wallace Karia amewaahidi wapiga kuwa wake kufanya kazi kwa weledi wa hali ya juu kwani nafasi aliyopewa na wajumbe hao kwa kumuamini ni deni ambalo atalilipa kwa kuleta mafanikio makubwa katika mchezo wa soka.
Bw. Karia alisema kuwa furaha waliyonayo viongozi wote waliochaguliwa kuiongoza TFF kwa muda wa miaka minne iende kuwa furaha ya kazi kwa kufanya yale watanzania wanatarajia kutoka kwao.