SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumapili, 6 Agosti 2017

T media news

Makosa 9 wanayofanya mabosi na kusababisha wafanyakazi wazuri kuondoka

Ni kitu kinachoshangaza ukiwasikia mameneja wakilalamika kuhusu wafanyakazi wao, na mara nyingine wanakuwa na sababu za msingi za kulalamika — ni vitu vichache sana vinavyowachanganya mabosi zaidi ya wafanyakazi bora kuwakimbia.

Mameneja huwa na tabia ya kulaumu vitu vingi sana juu ya kukimbiwa na wafanyakazi wao huku wakisahau au wakiwa hawajui kwamba watu hawakimbii ajira zao, wanakimbia mameneja.

1. Kuwapa rundo la kazi watu wake

Hakuna jambo linalowaudhi wafanyakazi wanaojituma zaidi ya kuwarundikia kazi kisa umegundua kuwa wanajituma sana. Mabosi wamekuwa wakishawishika kuwapa kazi nyingi wafanyakazi wao na wengi wamejikuta wanaingia kwenye mtego huu na kuishia kukimbiwa na wafanyakazi. Kuwapa wafanyakazi wako wanaojituma kazi nyingi sana inawafanya waone wanaadhibiwa kwa tabia yao ya kujituma. Kama ni lazima uongeze kazi kwa wafanyakazi wako wenye uwezo, ni bora ukawaongezea hadhi zaidi pia. Ongezeko la mshahara na cheo huwa inafanya kazi unazoziongeza zikubalike kirahisi zaidi.

Kama utakuwa unawaongezea kazi kwa sababu wana uwezo mkubwa wa kufanya kazi, bila kubadilisha lolote, wengi watajikuta wanatafuta kazi sehemu nyingine ambapo wanaweza kupata wanachotaka.

2. Kutothamini mchango na kazi kubwa inayofanywa

Ni rahisi sana kudharau jambo kama kumpa hongera mfanyakazi kwa kumgusa mgongoni inaweza kuwa na maana kubwa kiasi gani kwa mfanyakazi wako, hasa kwa wale wenye utendaji wa juu ambao huwa wanajituma wenyewe bila kusukumwa. Kila mfanyakazi anapenda pongezi toka kwa bosi wake, lakini wanaostahili zaidi pongezi hizi ni wale wanaojituma zaidi na kujitolea kufanikisha malengo ya kampuni.

Mabosi wanahitajika kuzungumza na wafanyakazi wao kujua nini kinachofanya kila mmoja aone anathaminiwa zaidi (kwa baadhi ni ongezeko la mshahara; kwa wengine, kuwapongeza mbele ya wafanyakazi wengine) na kisha kuwapa zawadi kwa kazi nzuri iliyofanywa. Kwa wafanyakazi wanaojituma, jambo hili utakuwa ukilifanya mara kwa mara kama ukiwa makini na kufatilia utendaji wao.

3. Kutojali wafanyakazi

Zaidi ya nusu ya wafanyakazi wanaoacha ajira zao wanafanya hivyo kwa sababu ya uhusiano kati yao na bosi. Makampuni yenye mafanikio zaidi yanahakikisha kuwa mabosi wanaoendesha kampuni hizo wana uwezo mkubwa wa kuhakikisha wafanyakazi wanafata taaluma lakini pia kuweka utu mbele kwenye uhusiano na wafanyakazi hao.

Kuna baadhi ya mabosi wanafurahia mafanikio ya wafanyakazi wao, kufariji walio kwenye matatizo, kuwapa changamoto na kuwaambia ukweli wafanyakazi wao, hata kama itawaumiza. Mabosi ambao hawajali maisha ya wafanyakazi wao watakimbiwa kwa kiwango kikubwa.

4. Kutotimiza ahadi anazotoa

Unapotoa ahadi kwa watu inakuweka kwenye nafasi ya kuwafurahisha sana au kusababisha waondoke kabisa. Unapotimiza ahadi zako, wafanyakazi wako wanakuongezea heshima zaidi kwa sababu unawathibitishia kwamba unastahili kuaminiwa na unatimiza kila unaloahidi (vigezo viwili vikubwa sana kwa kila bosi kuwa navyo). Lakini unapokuwa hutimizi ahadi zako ni rahisi kuonekana hujali, una dharau na huwaheshimu wafanyakazi wako.

Pia, wafanyakazi watajiuliza: kama bosi wetu mwenyewe hatimizi ahadi zake, kwanini sisi tumtimizie kazi zake?

5. Kuajiri na kuwapa vyeo wafanyakazi wasiostahili

Wafanyakazi wazuri na wenye juhudi wanapenda kufanya kazi na watu wanaofanana au waliowazidi uwezo. Endapo mabosi watazembea na kujikuta wanaajiri watu wenye uwezo mdogo, itafanya wafanyakazi wazuri kukosa msukumo wa kiushindani na kutoweka juhudi kazini.

Kuwapa vyeo watu wasiostahili au wenye uwezo mdogo ndio jambo baya zaidi. Kama unafanya kazi kwa ubunifu na uwezo wako wote na unaachwa kila msimu wa kupandishwa vyeo unapowadia na vyeo hivyo kupewa watu wenye uwezo mdogo zaidi ya ulionao, ­­­­­bila shaka utaona umedharauliwa kupita kiasi na yawezekana kabisa moja ya maamuzi utakayofikiria kuyafanya ni kuacha kazi hiyo.

6. Kutoruhusu wafanyakazi wao kufanya kazi wanayopenda

Wafanyakazi wenye vipaji na uwezo mkubwa huwa hawalazimishwi kufanya kazi, huwa wanajituma wenyewe. Kuwapa nafasi ya kufanya kazi kwa uhuru ili watumie ubunifu wao huwafanya waridhike. Lakini mabosi wengi wananataka watu wafanye kazi kwenye mazingira ya woga. Mabosi wa aina hii wanakuwa na hofu kwamba uzalishaji wa kampuni zao utapungua endapo watawaruhusu wafanyakazi wao wafanye mambo wanayoyapenda.

Hofu ya aina hii haina msingi wowote na cha zaidi itasababisha wafanyakazi wako kukimbia.

7. Kushindwa kuwaongezea watu mbinu bora za kufanya kazi

Pindi mabosi wanapoulizwa kuhusu mambo wasiyoyajua kuhusu wafanyakazi wao, wengi huwa wanatoa visingizio kama: “nawaamini,” “nimewapa uhuru kwenye kazi zao,” na “nawawezesha kujitegemea.” Hili ni suala baya kwakuwa mabosi wazuri huwa wanafatilia kila jambo kwa karibu na umakini, bila kujali mfanyakazi ana kipaji au uwezo mkubwa kiasi gani. Wanasikiliza wafanyakazi wao muda wote na kuwaambia athari ya kila wanachokifanya.

Ukiwa na wafanyakazi wenye vipaji au uwezo mkubwa, ni jukumu lako kama bosi kuwaangalia kwa umakini na kuwashauri wanapoweza kufanya maboresho ili waweze kupata matokeo bora zaidi. Wafanyakazi wenye uwezo mkubwa wanapenda wapewe mrejesho wa kazi wanayofanya — mara nyingi zaidi ya wale wenye uwezo mdogo au wa kawaida — na ni jukumu lako kama bosi wao kuwapa mrejesho huu. Kama hutafanya hivi, wafanyakazi wako wenye uwezo zaidi wataichukia kazi na hatimaye kukukimbia.

8. Kushindwa kutumia ubunifu wa wafanyakazi wao

Wafanyakazi wengi wenye vipaji, ubunifu na uwezo mkubwa zaidi huwa wanataka kuboresha kila kitu kwenye maisha yao. Kama ukiwaweka kwenye mazingira ambayo uwezo na ubunifu wao hauwezi kutumika kwa kiwango cha juu kwa sababu unaridhishwa na hali ya sasa, itawafanya waanze kuchukia ajira zao. Kuwazuia wasifanye ubunifu wao ni hakuathiri utendaji kazi wao tu, bali inaathiri utendaji wa taasisi au kampuni yako pia.

9. Kushindwa kuwapa wafanyakazi wao changamoto za kutosha

Mabosi wazuri wanawapa wafanyakazi wao changamoto ya kufanya kazi kwa bidii na ubunifu ili kuweza kufikia malengo ambayo mwanzo yawezekana yalionekana ni makubwa kupita kiasi na yasiyoweza kutimia. Badala ya kuweka malengo mengi madogo madogo, wao wanaweka malengo makubwa sana yanayofanya wajitume zaidi ya walivyokuwa wanafanya kabla.

Hivyo basi, ni wazi kuwa mabosi wazuri wanafanya kila jitihada zilizo ndani ya uwezo wao kuwasaidia wafanyakazi wao wapate mafanikio kwakuwa wafanyakazi wenye uwezo mkubwa kazini wanapojikuta wanafanya kazi nyepesi zisizo na changamoto kwao, watajikuta wanatafuta ajira sehemu nyingine ambazo zitawafanya watumie uwezo wao vizuri.

Kama unataka wachapakazi wako wabaki, yakupasa kufikiria vizuri na kuwa na mkakati wa kuwafanya wabaki kazini. Kwakuwa wafanyakazi wazuri huwa ni watu wenye msimamo sana na vipaji vyao vinawafanya wawe na wigo mpana wa kuchagua kazi, ni kazi yako kama bosi kuwafanya wapende kubaki na kufanya kazi na wewe.