SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumapili, 6 Agosti 2017

T media news

Rais Magufuli na Kagame ‘wachati’ Twitter

Ukuaji wa Sayansi na Teknolojia hasa katika nyanja ya Teknolojia, Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kunarahisisha mambo mengi sana ikiwa ni pamoja na kuwaunganisha watu waliopo maeneo mbalimbali duniani.

Urahisi huo unaweza kuonekana kwa namna ambavyo wananchi wamekuwa wakeleza matatizo yao kwa viongozi ambao wapo kwenye mitandao ya kijamii na kupatiwa ufumbuzi mara moja. Lakini mbali na hilo, viongozi wa nchi moja wamekuwa wakiwasiliana na viongozi wa nchi nyingine katika kuimarisha ushirikiano na ujirani baina hayo.

Kwa miaka ya nyuma, ingemlazimu kiongozi wa nchi ama kupiga simu, kuandika barua au kwenda mwenyewe anapotaka kumpongeza kiongozi mwingine kwa kushinda uchaguzi au jambo jingine jema alilofanya. Lakini ukuaji wa TEHAMA umerahisisha mambo hata Rais Magufuli akaweza kutuma salamu za pongezi kwa Rais Kagame kufuatia kushinda uchaguzi uliofanyika Agosti 4 nchini humo.

Baada ya Tume ya Uchaguzi ya Rwanda kumtangaza Kagame kuwa mshindi, Rais Magufuli kupitia akaunti yake ya Twitter aliandika ujumbe uliosomeka, “Nakupongeza Mhe. Paul Kagame kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Rwanda kwa kipindi kingine. Kwa niaba ya Watanzania wote nakutakia mafanikio mema. Tutaendeleza na kukuza zaidi ushirikiano na uhusiano kati ya nchi zetu hususani biashara na maisha ya wananchi wetu. Hongera Wanyarwanda.”

Baada ya kupata salamu hizo za pongezi kutoka kwa kiongozi mwenzake na rafiki yake, Rais Paul Kagame ambaye amechaguliwa kwa awamu ya tatu ambapo ataiongoza Rwanda kwa miaka 7 ijayo, alijibu ujumbe huo na kumhakikishia Rais Magufuli ushirikiano wa karibu kwa kipindi chote atakachokuwa madarakani.

Rais Kagame alipata ushindi wa kishindo baada ya kujizolea kura 98.63% ya kura zote halali. Wanyarwanda wengi wamempongeza kiongozi huyo wakisema kuwa ameleta maendeleo ya kiuchumi pamoja na kuifanya nchi hiyo kuwa imara.

Kwa mujibu wa ripoti ya Gallup ya mwaka 2017, imeitaja Rwanda kuwa ni nchi ya 2 Afrika na 11 duniani ambayo ni salama zaidi kwa binadamu kuishi.