SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumamosi, 12 Agosti 2017

T media news

Je Kunyonyesha Kuna Sababisha Maziwa ya Mwanamke Kudondoka? Huu Hapa Ukweli na Uongo Kuhusu Konyonyesha

Na Mary Mathenge

Maziwa ya mama yana virutubisho vyote kwa uwiano unaotakiwa kwa ajili ya ukuaji wa mtoto. Karibu wanawake wote wana uwezo wa kunyonyesha. Ni jambo ambalo mwanamke inabidi ajifunze na kujizoesha kabla halijawa jepesi kwake.

Uzushi mwingi unaosambaa kuhusu kunyonyesha umekuwa ukisambazwa kupitia kwa wanafamilia na marafiki lakini taarifa nyingine za aina hiyo hazina ukweli wowote au zimepitwa na wakati. Mary Mathenge ni Meneja wa Unyonyeshaji katika Chuo Kikuu cha Tiba Aga Khan jijini Nairobi anaelezea baadhi ya imani hizi za kizushi pamoja na kueleza usahihi wa jambo hilo.

UONGO KUHUSU KUNYONYESHA

Kunyonyesha kutasababisha matiti yadondoke

Kunyonyesha mtoto hakusababishi maziwa ya mama kuanguka. Kinachosababisha maziwa kuanguka ni kuongezeka kwa umri wa mwanamke, kupungua au kuongezeka kwa uzito wa mwili. Lakini pia, ni muhimu kwa mwanamke kuvaa sidiria sahihi ili kuyapunguzia uzito matiti ya mama anayenyonyesha kutokana na kuongezeka kwa maziwa yanayotakiwa kunyonywa na mtoto (uzito wa matiti huongezeka wakati wa kunyonyesha).

Maziwa ya kopo yana virutubisho sawa na vilivyomo kwenye maziwa ya mama

Virutubisho vinavyowekwa kwenye maziwa ya kopo havalingani na vilivyomo kwenye maziwa ya mama. Maziwa ya kopo hayatokani na kiumbe hai, kwahiyo hayana vimelea vya kuulinda mwili, seli hai, enzaimu au homoni ambazo zinamlinda mtoto wako asipate maambukizi na magonjwa mara kwa mara katika ukuaji wake.

Maziwa ya kopo yanatengenezwa kwa protini mbalimbali ikiwamo protini inayopatikana kwenye maziwa ya wanyama, soya na mafuta ya mimea. Na ingawa yameboreshwa ili kufananishwa na maziwa ya mama, bado maziwa haya ya makopo hayana uwezo wa kufananishwa kwakuwa hayatoki kwenye kiumbe hai kwenda moja kwa moja kwa mtoto.

Watoto wanaonyonya maziwa ya kopo wanakuwa na afya bora zaidi ya wale wanaonyonya maziwa ya mama

Watoto wanaonyonya maziwa ya mama zao wanaongezeka uzito kidogo baada ya mwaka mmoja ikilinganishwa na uzito mkubwa ambao huongezeka kwa watoto wanaonyonya maziwa ya kopo. Tafiti zinaonesha kwamba watoto walionyonyeshwa na mama zao si rahisi kuzidi uzito utotoni mwao au wanapokuwa watu wazima ikilinganishwa na watoto waliopewa maziwa ya kopo – pia huwa wanapata matatizo kidogo kiafya.

Watoto walionyonya maziwa ya kopo wanaweza kuwa na tatizo la kushindwa maziwa ya mama au ya mnyama ambayo yana protini kwa wingi, wana hatari kubwa zaidi ya kupata magonjwa ya kuharisha, matatizo ya tumbo, upele na magonjwa mengine kutokana na kunyweshwa maziwa yenye aina tofauti za protini.

Kunyonyesha ni rahisi kwa baadhi ya wanawake, lakini wengine hawatoi maziwa ya kutosha

Karibu wanawake wote kimaumbile wana uwezo wa kunyonyesha. Ni ujuzi ambao kila mwanamke anatakiwa kujifunza na kuufanyia mazoezi kabla hajazoea. Baadhi ya wanawake wanajifunza haraka na wengine huchelewa, lakini karibu wanawake wote wana uwezo wa kutengeneza maziwa ya kuwatosha watoto wao. Chakula anachokula mama anayenyonyesha huchukua nafasi kubwa sana katika utengenezwaji wa maziwa.

Wanawake wenye matiti madogo, hayatoi maziwa mengi

Umbo na ukubwa wa matiti na chuchu za mzazi unatokana na kiwango cha mafuta tishu zilizopo kwenye maziwa, hivyo, mwanamke awe na matiti makubwa au madogo, bado wana uwezo wa kuwa na maziwa mengi ya kutosha.

Mwenye chuchu ndogo au zilizoelekea juu hawezi kunyonyesha

Baada ya kujifungua, wanawake wengi wenye chuchu ndogo au zilizoelekea juu wataona mabadiliko ambapo chuchu zake zitajirekebisha mara baada ya kuanza kunyonyesha – hakuna matayarisho yoyote yanayotakiwa kufanywa wakati wa ujauzito. Mazoezi yanayofanywa na wengi ya kuvuta na kuzungusha chuchu za matiti hayasaidii chochote.

Wanaonyonyesha wanapunguza uwezekano wa kubeba mimba tena

Kumnyonyesha mtoto mchanga kunamsaidia mwanamke. Kunyonyesha ni njia ya asili ya kupanga uzazi inayosaidia sana mtoto anapokuwa chini ya miezi sita kwakuwa anakuwa mzazi anakuwa anatumia muda mrefu kumnyonyesha mtoto na bado mzunguko wa hedhi unakuwa haujaanza rasmi. Kunyonyesha kunasaidia kuchelewa kurutubishwa kwa mayai, lakini ufanisi wa njia hii ya kupanga uzazi huondoka mtoto kunyonya kidogo na kulala zaidi. Kwahiyo, kama mzazi hataki kupata mimba anatakiwa kutumia njia nyingine salama zaidi ya uzazi wa mpango mapema anapoanza tena kujamiiana baada ya kujifungua.

Mama anayenyonyesha hawezi kufanya mapenzi kwa njia salama

Baada ya kujifungua, utaamua mwenyewe uanze lini uanze tena kujamiiana na mwenza wako. Aina ya homoni inayosaidia kuruhusu maziwa kutoka ili yanyonywe na mtoto (xytocin) hutengenezwa pia wakati wa kujamiiana. Hivyo wakati wa kujamiiana, mwanamke anaweza kutokwa na maziwa kidogo – hili ni jambo la kawaida, usishangazwe nalo.

Watu hawapendi kuona mwanamke akinyonyesha hadharani

Tafiti zinaonesha kwamba watu wengi hawashangazwi na hawakerwi kuona mwanamke anamnyonyesha mwanaye hadharani. Sanasana watu watamkasirikia na kumkaripia mzazi ambaye anamwacha mtoto alie muda mrefu kwa njaa akihofu kuonekana. Watoto wanatakiwa kunyonya kila mara, na hii inamaanisha mama anakosa sehemu ya faragha ya kumnyonyesha mtoto.

Mzazi anatakiwa kuvaa nguo zinazoweza kumfanya anyonyeshwe kirahisi, kama sidiria maalum za kunyonyeshea au nguo inayoweza kupanda juu kwa urahisi kutokea kiunoni au inayoshuka kirahisi kutokea juu. Pia ni vizuri kuwa na kitambaa chepesi au mtandio kwa kujifunika kuzunguka mabega ili kujisitiri.

UKWELI KUHUSU KUNYONYESHA

Watoto wanaweza kuishi kwa kunyonya maziwa ya mama tu kwa miezi sita ya mwanzo

Inashauriwa kwamba watoto wapewe maziwa ya mama tu katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo toka kuzaliwa. Maziwa ya mama yana virutubisho sahihi katika uwiano unaotakiwa kwa ajili ya ukuaji wa kawaida wa mtoto mpaka atakapofikisha umri wa miezi sita. Maziwa ya mama ni rahisi kumeng’enywa, yanatumiwa kwa kiasi kikubwa mwilini, masafa, yana joto linalotakiwa na binadamu na si rahisi kupata maambukizi kabla mtoto hajayanyonya na pia yanaondoa uwezekano wa mtoto kuwa na uzito mkubwa sana utotoni mwake.

Kunyonyesha kunamsaidia mama kupunguza uzito ulioongezeka wakati wa ujauzito

Sio tu kwamba kunyonyesha kunamsaidia mwanamke kupunguza uzito wa ziada (ulioongezeka wakati wa ujauzito), pia inasaidia kufanya mji wa uzazi kurudi katika hali yake ya kawaida na kupunguza kiasi cha damu inayotoka katika wiki sita za kwanza toka kujifungua (kipindi ambacho maumbile ya mzazi yanarudi kwenye hali yake ya kawaida yalivyokuwa kabla ya ujauzito).

Mtoto anatakiwa kunyonyeshwa haraka iwezekanavyo baada ya kuzaliwa

Haraka sana baada ya kuzaliwa (ikiwezekana kabla ya kitovu kukatwa), mtoto anatakiwa anyonyeshwe na kisha anyonye mara kwa mara anapopata njaa. Mara nyingi mtoto ananyonya maziwa mengi katika saa mbili za kwanza tangu azaliwe. Kwa wale waliojifungua kwa upasuaji, mama anatakiwa apewe mwanaye mara moja baada ya kutoka kwenye chumba cha upasuaji (hasa katika upasuaji ambao mama anakuwa hajapewa dawa za usingizi au kupoteza fahamu) ili aweze kumnyonyesha mtoto.

Mtoto anapokataa kunyonya

Kama mtoto atakataa kunyonya, basi yawezekana ni kwa sababu ana vidonda mdomoni ambavyo anaweza kuvipata wakati mama anajifungua. Pia, mtoto anaweza kuwa amezaliwa akiwa anaumwa lakini jambo kama hili linapotokea inatakiwa lichunguzwe na kupatiwa matibabu. Muda mwingine sababu yawezekana mzazi anakuwa na maziwa mengi sana na yanayotoka kwa kasi hadi kumpalia mtoto wakati ananyonya. Ikiwa ni hivi, ni vyema mama akakamua na kuhifadhi maziwa haya kwenye chombo safi na kuyaweka kwenye friza ili yatumike baadaye.

Chuchu za mama zinapouma, ni ngumu kunyonyesha

Maumivu kwenye chuchu yanatokea iwapo mtoto atawekwa vibaya kwenye titi la mama. Mtoto anatakiwa kuingiza mdomoni sehemu ya titi la mama, sio chuchu peke yake. Kama ikifanyika hivi, chuchu za mama hazitakiwi kuuma, hata kwa siku za mwanzo za kunyonyesha. Mafuta-salama yanayomsaidia mzazi aendelee kumnyonyesha mtoto hata kama chuchu zinauma.

Mzazi anayefanyakazi pia anaweza kumpa mwanae maziwa tu kwa miezi sita ya mwanzo

Mzazi anaweza kuendelea kumpa mwanaye maziwa tu kwa miezi sita ya mwanzo au zaidi akiwa ameajiriwa. Anaweza kumnyonyesha moja kwa moja nyakati anazokuwa nyumbani baada ya muda wa kazi na kukamua maziwa na kuyahifadhi ili anyweshwe wakati anapokuwa kazini. Maziwa haya yanaweza kuhifadhiwa na mtoto kuyanywa siku inayofata.

Maziwa haya yaliyokamuliwa kutoka kwenye matiti ya mzazi yanabaki kuwa salama kwa mtoto yakihifadhiwa kwa muda wa saa nane kwenye joto la kawaida la nyumbani. Pia yanaweza kuhifadhiwa kwa kugandishwa kwenye friza kwa miezi sita na kuwa salama kwa mtoto. Chombo kilichogandisha maziwa hayo kinatakiwa kiwekwe kwenye maji ya moto ili maziwa yaweze kuyeyuka taratibu.