SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Ijumaa, 21 Julai 2017

T media news

BIDHAA za Tanzania zafutiwa Kodi China

Kiwango cha biashara kati ya Tanzania na China kimefikia Dola bilioni 4.7 katika kipindi cha mwaka 2015 na kwamba kiwango hicho kinatarajiwa kuongezeka zaidi.

Mwakilishi Mkuu Mkazi wa Masuala ya Uchumi na Biashara, katika Ubalozi wa China hapa nchini, Bw. Lin Zhiyong, amesema hayo Jijini Dar es Salaam, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya forodha kuhusu maboresho na Vihatarishi vya kiforodha, yanayotolewa kwa maafisa wa forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na wataalamu kutoka Chuo cha Forodha cha Shanghai-China.

Bw. Lin Zhiyong amesema hivi sasa nchi yake ni kama imeondoa kabisa kodi kwa bidhaa za Tanzania zinazosafirishwa kwenda China hadi kufikia 97% na kwamba anatarajia kuona wafanyabishara wa Tanzania wakichangamkia fursa hiyo na kuongeza kiwango cha bidhaa za Tanzania zenye ubora zinazosafirishwa kwenda nchini China.

Mbali na hilo Zhiyong amedai hivi karibuni China iliipatia Tanzania seti 3 za makontena ya vifaa vya kisasa kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa mizigo katika bandari ya Dar es Salaam, vyenye uwezo mkubwa wa kugundua pembe za ndovu, dawa za kulevya na silaha zinazosafirishwa kimagendo kutoka ndani na nje ya nchi.