Hatimaye Mzee Said Mohamed Abeid, amezikwa leo November 8 kwenye makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam huku viongozi na wadau wengi wa soka wakijitokeza kumsindikiza katika safari yake ya mwisho.
Mzee Said Mohamed Abeid, alifarikiki jana alasiri katika Hospitali ya Agakhan jijini Dar es Salaam ambako alikuwa akipatiwa matibabu.
Mzee Said Mohamed, atakumbukwa kama mmoja wa nguzo muhimu kwenye mafanikio ya klabu ya Azam FC tangu kuanzishwa kwake miaka takribani nane iliyopita.
Chini ya uongozi wake kama Mwenyekiti wa Azam FC, aliiongoza klabu hiyo kunyakuwa mataji mbalimbali makubwa na kwa mafanikio, ikiwemo taji la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la Mapinduzi (mara mbili) pamoja na Ngao ya Jamii.
Si hivyo tu, mchango wake Mzee Said Mohamed haukuishia kwenye klabu ya Azam FC, bali hata kwenye familia ya soka la Tanzania kwa ujumla wake ambapo hadi umauti unamkuta alikuwa ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Luu Tanzania Bara na Mjumbe wa Kamati mbalimbali za Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF).
Mwenyezi Mungu ailaze roho yake Said Mohamed Abeid mahali pema peponi, Amiin,
Innalilah Wa-inna-ilaih Rajioun.