Kocha msaidizi wa Simba Jackson Mayanja amesema wamejisikia furaha kubwa kutokana na ushindi wa mabao 2-0 waliopata kwenye mchezo wa jana wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City uliofanyika Uwanja wa Sokine jijini Mbeya.
Mayanja amesema hakikuwa kitu rahisi kupata ushindi hasa ikizingatiwa kwamba walikuwa wakicheza na timu ngumu tena kwenye uwanja wa ugenini, hivyo ushindi huo ni kitu kikubwa sana kwao.
“Sisi kama Simba tumejisikia vizuri sana kupata ushindi wa ugenini japokuwa haikuwa rahisi sana lakini tumeweza kupata ushindi wa magoli mawili, ni kitu izuri sana kwetu kwasababu inatuweka kwenye nafasi nzuri na kuongeza chance (nafasi) yetu ya kumaliza kileleni kwenye raundi ya kwanza,” Mayanja alisema.
Ameongeza kuwa mfululizo wamatokeo mazuri kwa timu yao ni muenedelezo wa mashikamano uliopo klabuni hapo hivyo kuongeza ari kwa wachezaji.
“Umoja na ushirikiano mzuri uliopo baina ya mashabiki, viongozi, wachezaji na benchi la ufundi ndiyo mafanikio yatimu yetu kwa sasa.”
“Mbeya City si timu mbaya, ni timu nzuri na wamekuwa wakicheza vizuri kwenye kila mechi isipokuwa tumekuwa bora zaidi yao ndiyo maana tukapata ushindi.”
“Katika mchezo huu lengo letu lilikuwa ni kuanza kwa kasi ili tuue mchezo mapema na baadaye tuweze kucheza mpira wetu tuliozoea.”
Alipoulizwa kuhusu kufanya mabadiliko ya baadhi ya wachezaji waliocheza mchezo wa jana, Mayanja alijibu: “Simba ina kikosi kipana, kila mchezaji aliye kikosini ana nafasi ya kucheza kutokana na kuwa na viwango sawa, Simba ya mwaka huu sio ile ya miaka mitatu nyuma, safari hii kila mchezaji ana nafasi.”