Na Baraka Mbolembole
BAADA ya kufanikiwa kupanda daraja, kutoka ligi daraja la saba hadi daraja la sita, Kilimanjaro FC-timu iliyoanzishwa na Watanzania nchini Sweden inakusudia kuongeza nguvu katika kikosi chao kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi daraja la 6 nchini humo.
Timu hiyo imeanzishwa kwa lengo la kuwasaidia wanasoka wa Afrika Mashariki siku zijazo kucheza soka barani Ulaya.
“Mikakati yetu ni kujiimarisha zaidi ili ikifika mwezi April mwaka ujao ligi itakapoanza tufanye vizuri zaidi ya ilivyokuwa katika ligi daraja la saba. Malengo yetu ni kutoka daraja la sita twende ligi daraja la tano,” anasema mchezaji wa timu hiyo, Shekhan Rashid nilipofanya naye mahojiano akiwa nchini Sweden.
“Tumejipanga kufanya maandalizi mapema, maana kila kitu kipo sawa, zaidi tunaomba Mungu tu atujalie atujalie uzima. Tutaangalia uwezekano wa kuongeza baadhi ya wachezaji kama watatu ambao ni Watanzania wako hapa Sweden ila hawakuwa na usajili. “
“Usajili wao utatuimarisha maana sasa ni ngumu kusajili mchezaji kutoka Tanzania, sheria hairuhusu. Kuanzi ligi daraja la 3 hadi ligi kuu ndiyo tunaweza kuleta wachezaji kutoka nje,” anasema Shekhan mchezaji wa zamani wa Simba SC, Mtibwa Sugar, Moro United na Azam FC za hapa Tanzania.
“Tunawaomba Watanzania waendelee kutusapoti na tunawashukuru sana kwa sapoti yao maana hii timu malengo yetu ni kuja kuwawekea njia wadogo zetu kurahisha wapate nafasi ya kucheza huku.”
“Kama nilivyokwambia, tukifika kuanzia daraja la tatu tunaruhusiwa kuleta wachezaji kutoka Tanzania kwani tutakuwa katika ligi za kulipwa na itakuwa faida kubwa sana kwa timu yetu ya Taifa.”
“Hakuna kingine, tunafanya hivi kusaidia Watanzania wenzetu. Furaha yangu na wenzangu waliopo huku ni kuja kuona watu wanafaidika na matunda yetu. Mungu atatusimamia kwa hili.”