JITIHADA za Rais John Magufuli katika kubana matumizi yasiyo ya lazima serikalini, ambazo alizihamishia katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ikiwamo kuzuia safari zisizo za lazima katika jumuiya hiyo, zimewezesha kuokoa zaidi ya Sh bilioni 1.2.
Rais Magufuli ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na aliahidi kuchukua hatua za kubana matumizi yasiyo ya lazima na ikibidi kutumbua watendaji wa EAC, baada ya kuchaguliwa kushika wadhifa huo Machi mwaka huu jijini Arusha.
Katibu Mkuu wa EAC, Balozi Liberat Mfumukeko alisema jana jijini hapa kuwa jitihada za kubana matumizi yasiyo ya lazima, zimeokoa Dola za Marekani 588,768 (zaidi ya Sh bilioni 1.2) ndani ya kipindi cha miezi mitatu kuanzia Mei hadi Agosti mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari kwa mara ya kwanza tangu ashike wadhifa huo Aprili mwaka huu, Balozi Mfumukeko alisema kiasi hicho cha fedha kiliokolewa kutokana na kubana safari zisizo za lazima za watumishi na watendaji wa jumuiya katika kipindi hicho.
“Utekelezaji wa ubanaji wa matumizi yasiyo ya lazima unategemewa kuokoa dola za Marekani milioni sita kwa mwaka huu wa fedha 2016/2017 na tutakuwa tunatoa taarifa hizi kwa watu wa Afrika Mashariki kila baada ya muda,” alisema Balozi Mfumukeko ambaye ni Katibu Mkuu wa Tano wa EAC.
Kuhusu mafanikio ya utekelezaji wa makubaliano mbalimbali ya jumuiya hiyo, Balozi Mfumukeko alieleza kwamba utekelezaji unaendelea vyema pamoja na changamoto mbalimbali zinazojitokeza.
Alisema katika utekelezaji wa kuwa na vituo vya ukaguzi wa mizigo vya pamoja mipakani, vituo 10 kati ya 15 vinatekeleza ukaguzi huo kwa mafanikio na kupunguza gharama za kufanya biashara.
“Kutokana na vituo hivyo kuanza kazi, hivi sasa kusafirisha mizigo kutoka Mombasa hadi Kampala inachukua siku nne badala ya siku 20 za awali, jambo linalowasaidia wasafirishaji kupunguza gharama za kufanya biashara,” alisisitiza.
Tangu alipoingia madarakani, Rais Magufuli amedhibiti mianya ya rushwa ikiwemo kupunguza safari za nje pamoja na kutumbua majipu mbalimbali kwa nia ya kubana matumizi sanjari na kuhakikisha kila mtu ananufaika na matunda ya nchi yake pamoja na kurejesha heshima ya kazi kwa watumishi wa umma.