SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Alhamisi, 22 Septemba 2016

T media news

Matarajio na uhalisia wa Oktoba 1

Na Ayoub Hinjo

Ndugu msomaji,hakuna asiye fahamu kuwa siku za hivi karibuni kutakuwa na mechi ya watani wa jadi hapa Tanzania,Simba na Yanga. Ni mechi ambayo imeteka hisia za wapenda soka wengi hapa nchini na nchi za jirani,hii ni mechi kubwa mno kwenye soka la Tanzania.

Kwa bahati mbaya naweza sema matarajio ambayo yapo kwa mashabiki kuelekeo mchezo huo ni makubwa kuliko uhalisia ambao watakutana nao siku ya pambano hilo. Matarajio ya wengi ni kuona mechi iliyojaa ufundi,yenye burudani na yenye kutoa funzo kwa timu zingine.

Matarajio mengine ni kushuhudia nidhamu kwa timu zote mbili, kushuhudia mchezo wa uungwana uliojaa weledi wa hali ya juu. Matarajio ni mengi sana na matarajio yote yana asilimia chache kutimia sababu uhalisia ndio utafunika matarajio hayo.

Uhalisia ndio utatawala zaidi ya matarajio ya mashabiki. Uhalisia wa kuelekea mechi hiyo tunaweza kushuhudia mchezo uliojaa vurugu,mchezo uliojaa visa na usio na burudani. Mara zote huwa ni mchezo uliokosa nidhamu. Maandalizi ya kuelekea mchezo huo hayafanani kabisa na uhalisia ambao unatokea uwanjani.

Matarajio ya nje ya uwanja yanapotezwa na uhalisia wa ndani ya uwanja. Ni mara chache sana kuona matarajio na uhalisia vikifanana na kutimiza kile mashabiki walichokitarajia.

Kitu cha ziada kuelekea mchezo huo ni pale tunapoona mchezo wa watani wa jadi nchini umekosa matangazo ya kutosha kwenye vyombo vya habari na hata kwenye mitandao ya kijamii. Kwa nchi zilizoendelea kisoka mechi kama hii ni chanzo cha pesa kwa timu zote mbili kuingia makubaliano ya kurusha matangazo au kuwa chanzo cha kutangaza biashara za timu husika ili kuvuta hisia za mashabiki kuelekea mchezo huo.

Acha tuendelee kuwa na matarajio kuelekea mchezo huo wa Oktoba 1 na tuendelee kuomba uhalisia ufanane na matarajio tunayoyataka. Lazima tubadilike sababu michezo ya aina hiyo ndio kioo kwa timu zingine kujifunza zaidi na mara nyingi inakuwa kivutio hata kwa nchi zingine.