SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumanne, 13 Septemba 2016

T media news

Jinsi muziki wa Singeli ulivyogeuka dhahabu ndani ya kipindi kifupi

Nilianza kuusikia muziki wa Singeli mwaka na nusu uliopita na zaidi kwenye Bajaj nilizokuwa napanda. Sikuuelewa kabisa muziki huu na mara nyingi niliona ukinipigia kelele tu.

Nilikuwa najiuliza ni kipi hasa watu hawa walikuwa wanaimba na tena wakiwa na mfumo na njia zao wenyewe. Ni kama vile walipita shule moja na kujifunza uimbaji wake. Ama hakika muziki huu ulikuwa ukinishangaza sana. Kwa wengi pia muziki huu ulionekana wa vijana wahuni wanaoishi maeneo ya uswahilini. Lakini watu wanaojua, wanasema umekuwepo mtaani kwa zaidi ya miaka 10 sasa na ulikuwa maarufu kwenye sherehe za uswazi kama vile vigodoro na zingine.

Ni muziki ambao wakati mwingi ulikuwa ukiimbwa na wahuni, vibaka, wavuta bangi na wengine mateja. Kwa mujibu wa Kicheko, mtu muhimu kwenye muziki huo, Singeli ni muziki uliokuwa ukiimba na vijana waliokuwa na stress na ulitumika kama njia ya kuzipunguza.

Miaka mitatu iliyopita, hakuna kituo cha redio kilichokuwa kinautambua muziki huu kama wenye kiwango na ubora wa kuchezwa hewani. Japokuwa kulikuwa na muziki wa uswazi kama mnanda wa wasanii kama Omari Omari uliopenya mainstream, muziki wa Singeli ulianza kuchezwa zaidi miaka miwili iliyopita.

Na hakuna anayeweza kubisha kuwa EFM wamekuwa na mchango mkubwa sana kwenye ukuaji na kisha kukubalika kwa Singeli. Wao walitenga kabisa vipindi vya kucheza muziki huo kikiwemo Genge. Lakini pia EFM ilikuwa ikicheza muziki huo hata kwenye vipindi vya asubuhi (Breakfast show), kitu ambacho hakuna redio iliyokuwa ikifanya hivyo.

“Heri ya kuzaliwa kaka mkubwa !! @majizzo naweza kusema wewe kwa binafsi yako una mchango mkubwa kwenye mziki wetu wa #singeli,” aliandika nyota wa Singeli Sholo Mwamba alipokuwa akimpongeza CEO wa EFM, Majay kwenye siku yake ya kuzaliwa.

Katika kipindi hiki kifupi muziki wa Singeli umezalisha mastaa wakiwemo Sholo Mwamba na aliyekuwa Dj wake, Man Fongo. Lakini pia wasanii wa Bongo Flava kama Rama Dee na Profesa Jay wametoa nyimbo zao wakiwashirikisha waimbaji wa Singeli, Young Yuda na Sholo Mwamba.