SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumanne, 13 Septemba 2016

T media news

Sanamu mpya za Mugabe zazua ubishi Zimbabwe

Sanamu mbili mpya za kiongozi wa muda mrefu wa Zimbabwe Robert Mugabe zimezinduliwa mjini Harare.

Sanamu hizo, ambazo zilizinduliwa katika ikulu ya rais zimetayarishwa na mchongaji sanamu maarufu Dominic Benhura.

Rais Mugabe ameeleza kufurahishwa na sanamu hizo mbili kwa mujibu wa gazeti la serikali The Herald.

"Hii ni kazi nzuri Sanaa ya Sanaa na wasanii walioshiriki inaonekana wana vipaji adimu, wana vipaji kwa kweli," amenukuliwa Bw Mugabe.

Bw Benhura ameoneshwa kwenye picha zilizochapishwa na gazeti la The Herald akiwa amesimama karibu na sanamu hiyo akiwa na Bw Mugabe na mke wa rais Dkt Grace Mugabe.

Sanamu hiyo, ambayo urefu wake ni karibu maradufu kimo cha Rais Mugabe, inamuonesha kiongozi huyo wa umri wa miaka 92 akiwa na miwani yake maarufu, masharubu na akiwa ameinua mkono akiwa ameufumbata kama ngumi.

Baadhi ya raia nchini Zimbabwe hata hivyo hawajapendezwa na sanamu hizo na wanasema zinaonekana kama vibonzo.

"Robert Mugabe ametukanwa kwa sanamu hii na bado hajaelewa," mmiliki wa gazeti ambaye pia ni mwanaharakati Trevor Ncube ameandika kwenye Twitter.

"Ningelikuwa Robert Mugabe yule mtawala wa kiimla, ningeamuru (Benhura) akamatwe na niue sanamu hizo."

Wengine hata hivyo wamemtetea, akiwemo waziri wa sayansi Jonathan Moyo ambaye ameandika kwenye Twitter: "Wachongaji vinyago Zimbabwe wana uhuru wa kisanaa. Mvuto wa sanaa umo kwenye anayetazama. Benhura ni mchongaji vinyago anayeheshimika!"

Msanii huyo, ambaye anasema ilimchukua miezi sita kutengeneza sanamu hizo za Bw Mugabe, pia amejitetea.

"Nilipokea wajibu huu na nikafanya kadiri ya uwezo wangu. Kawaida, kazi yangu si kutengeneza picha (kazi za Sanaa) za kuashiria sura za watu. Bila shaka, hazikutokea kama wengi walivyotarajia," Benhura ameambia shirika la habari la AFP, Bw Mugabe ameongoza Zimbabwe tangu 1980.