SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumanne, 13 Septemba 2016

T media news

Dk Shein alia mgawanyiko Z’bar

Zanzibar. Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein alitumia maadhimisho ya ibada ya Eid el Hajj kuwataka Wazanzibari kuwa wamoja huku mgawanyiko mkubwa baina ya Unguja na Pemba ukiendelea kujidhihirisha.

Akihutubia waumini wa dini ya Kiislamu jana katika Baraza la Eid el Hajj lililofanyika Mkoani, Pemba Dk Shein alisema hali ya mgawanyiko inayooekana hivi sasa haileti taswira nzuri kwa nchi. Dk Shein alihutubia Baraza la Eid ambalo halikuhudhuriwa na viongozi wa CUF kwa madai hawakualikwa.

Rais Shein alisema katika siku za hivi karibuni vitendo vya kutengana vimekuwa vikionekana waziwazi huku wengine wakichomeana nyumba na kuharibiana mazao jambo ambalo linatishia hali ya uvunjifu wa amani nchini.

“Hali ya kuwepo kwa mizozo na mivutano kwa baadhi ya mashehe na waumini inayotokana na misimamo yao, nayo inaweza kusababisha mifarakano katika jamii,” alisema.

Kauli ya CUF
Akitoa salamu za Eid kwa waumini baada ya kuswali katika Msikiti wa Kiembesamaki, Unguja, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad aliwataka wananchi kuwa na subira na kutovunjika moyo kwani hakuna jambo lisilo kuwa na mwisho wake.

Pia, alitoa pole kwa ndugu na jamaa kutokana na msiba janga la tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera na kusababisha vifo vya watu 16 na majeruhi 250.

Kuhusu sababu za kutohudhuria Baraza la Eid lililofanyika Mkoani, Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano Umma wa CUF, Salim Bimany alisema hakuna mwaliko uliofikishwa katika ofisi ya chama hicho kwa ajili ya sala hiyo.