SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatatu, 18 Aprili 2016

T media news

Kongamano la usalama barani Afrika lafanyika mjini Addis Ababa, Ethiopia

Kongamano la usalama barani Afrika lenye kaulimbiu ya 'Afrika katika Ajenda ya Usalama wa Dunia' na lenye lengo la kubadilishana mawazo na kuchunguza changamoto za usalama hususan vitisho vya ugaidi, lilianza hapo jana Jumamosi mjini Addis Ababa mji mkuu wa Ethiopia.

Katika kongamano hilo la siku mbili ambalo limesimamiwa na Taasisi ya Utafiti kwa ajili ya Usalama na Amani iliyo chini ya Chuo Kikuu cha Addis Ababa na kuhudhuriwa na viongozi wengi wa nchi za Afrika, washiriki wamejadili kwa kina changamoto za usalama hivi sasa barani humo. Miongoni mwa mambo mengine yaliyojadiliwa katika kongamano hilo la ushirikiano, ni kuandaa mipango ya kudhamini usalama na amani barani Afrika sanjari na kupambana na umasikini. Ukweli ni kwamba suala la usalama hivi sasa limegeuka na kuwa tatizo kubwa kwa nchi za Kiafrika, ambapo ugaidi umekuwa jinamizi kwa nchi zote za dunia. Utajiri mkubwa wa nchi za Kiafrika, kuwepo viongozi dhaifu, hali mbaya ya kisiasa na nafasi maalumu ya kijografia, kukosekana nafasi za kazi na pato dogo kwa vijana ni mambo yaliyochangia makundi ya kigaidi kueneza shughuli na ushawishi wao barani humo. Kwa mujibu wa weledi wa mambo, nafasi ya kisiasa na kiuchumi ya bara la Afrika ni jambo ambalo kwa muda mrefu limezivutia nchi za kikoloni na kuzifanya zipenye na kujiingiza barani humo. Nchi hizo ziliingia katika bara hilo kwa kisingizio cha kutoa misaada na kuzisaidia tawala za ndani, suala ambalo lilikuwa ni sawa na kukabiliana moja kwa moja na watu wa bara hilo. Aidha wakati mwingine wakoloni walijipenyeza ndani ya nchi hizo kwa kuwasha moto wa hisia za ukabila na kidini suala ambalo lilizitumbukiza nchi nyingi katika vita vya ndani, huku wakoloni wakitumia vibaya mazingira hayo kujinufaisha kwa kuuza silaha zao na kujineemesha kiuchumi kupitia damu za Waafrika. Hii leo pia wakoloni haohao kupitia ukoloni mamboleo, wanaendeleza ukoloni wao ndani ya baadhi ya nchi za Kiafrika kwa kuunga mkono na kuwalinda viongozi waliowaingiza madarakani. Mbali na wakoloni wa Kimagharibi, hivi sasa bara la Afrika linakodolewa macho pia na mataifa mengine. Nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi ikiwemo Saudia ambayo imeshindwa kufikia malengo yake haramu katika nchi za eneo la Mashariki ya Kati, sasa imeamua kujipenyeza barani Afrika kupitia kuibua tofauti au kutoa misaada ya kifedha na silaha kwa makundi ya kigaidi na kitakfiri. Kwa muda mrefu sasa bara la Afrika limekuwa likikodolewa macho na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, ambapo kupitia mbinu tofauti kama vile kupanua wigo wa kibiashara na misaada tofauti ya kiuchumi, umeweza kupenyeza katika baadhi ya nchi za bara hilo. Katika upande mwingine licha ya kwamba nchini nyingi zilizostawi kisiasa zimeanza kupiga hatua katika ustawi wa kidemokrasia, lakini kutokana na utendaji wa viongozi wengi wa bara hilo kukumbatia mienendo yao ya zamani sanjari na kubadili katiba, wakaazimia kuendelea kusalia zaidi madarakani ndani ya nchi zao. Masuala hayo pamoja na mengine ndiyo yamepelekea kushadidi migogoro ya kijamii na kisiasa katika nchi za bara hilo ambapo kwa upande mmoja yameibua malalamiko ya kila siku ya wananchi na kwa upande wa pili kuchochea ukandamizaji wa viongozi dhidi ya wananchi wao. Kukosekana uthabiti wa kisiasa ndani ya mataifa hayo kumetoa fursa kwa makundi ya upinzani na wanamgambo, kuweza kubeba silaha na kuchafua usalama wa nchi hizo katika kutaka kufikia malengo yao kupitia vitendo vya ukatili na mauaji. Katika sehemu nyingine makundi hayo yamebadilika na kuwa ya kigaidi ambapo sasa yanadai umiliki wa ardhi. Hivi sasa kundi la kigaidi na kitakfiri ka Boko Haram huko magharibi mwa Afrika limegeuka na kuwa tishio kubwa kwa nchi za eneo hilo na hata kwa ulimwengu kwa ujumla. Hayo yakiwa hivyo huko magharibi mwa Afrika, kundi la ash-Shabab na al-Murabitun yameharibu usalama wa nchi nyingine za bara la Afrika. Ni kwa kutilia maanani hayo ndipo nchi za Kiafrika zikaamua kushiriki kongamano la usalama lenye kaulimbiu ya 'Afrika katika Ajenda ya Usalama wa Dunia' ili kuweza kuyapatia ufumbuzi masuala hayo na mengine mengi.