SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatatu, 28 Machi 2016

T media news

Mvutano katika uhusiano wa Rwanda na Burundi


Mvutano katika uhusiano wa Rwanda na Burundi
Chama tawala Burundi kimemtuhumu Rais wa Rwanda kuwa anatekeleza maangamizi ya kizazi. Paschal Nyabenda mkuu wa chama tawala cha Burundi CNDD-FDD ameashiria maangamizi ya kizazi yaliyojiri Rwanda na kueleza kuwa Rais Paul Kagame wa nchi hiyo anawasajili vijana wa Burundi katika kambi za wakimbizi zilizopo Rwanda na kuwapatia mafunzo, ili baadaye wakirejea nchini kwao watekeleze mauaji ya kimbari.
Mkuu wa chama tawala nchini Burundi pia amezituhumu baadhi ya serikali za Ulaya kuwa zinampatia silaha na fedha Rais wa Rwanda kwa lengo hilo hilo. Hii ni mara nyingine ambapo Burundi inaituhumu Rwanda kuwa inawapa mafunzo ya kijeshi wakimbizi wa nchi hiyo ili baadaye wakirudi Burundi watekeleze oparesheni za kijeshi.
Raia wa Burundi zaidi ya laki mbili na nusu wamekimbilia nchi jirani ikiwemo Rwanda, kufuatia kupamba moto hali ya mchafukoge na mivutano ya kisiasa nchini Burundi. Serikali ya Bujumbura inawatuhumu vioongozi wa serikali ya Rwanda, khususan Rais Rais Paul Kagame mwenyewe kuwa wanaingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo na kufanya kila wawezalo ili kumuondoa madarakani Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi.
Kabla ya hapo na baada ya serikali ya Burundi kutoa madai hayo, Umoja wa Mataifa uliamua kutuma ujumbe wa wataalamu wake nchini humo ili kufanya uchunguzi zaidi. Uchunguzi huo umethibitisha suala hilo, hata hivyo viongozi wa Rwanda wameutaja utafiti huo kuwa ni wa uwongo.
Siku kadhaa zilizopita pia Wizara ya Mambo ya Ndani na Masuala ya Uzalendo ya Burundi ilitangaza kuwa inajiandaa kufungua mashtaka dhidi ya serikali ya Rwanda na Rais Paul Kagame wa nchi hiyo ambayo yatawasilishwa kwa taasisi za kisheria za kimataifa.
Mapigano nchini Burundi yalianza mwanzoni mwa mwezi Februari mwaka jana kufuatia hatua ya Pierre Nkurunziza ya kugombea tena kiti cha urais kwa muhula wa tatu. Licha ya kutekelezwa jitihada za kimataifa kwa minajii ya kuhitimisha mgogoro owa Burundi, lakini juhudi hizo hadi sasa zimeshindwa kuzaa matunda. Benjamin Mkapa Rais mstaafu wa Tanzania siku kumi zilizopita alielekea Burundi akiwa kama mkuu wa kundi la usuluhishi katika mgogoro wa nchi hiyo na kufanya mazungumzo na Rais Pierre Nkurunziza. Baada ya mazungumzo hayo, Mkapa alisema kuwa anataraji kwamba machafuko na mzozo wa ndani unaoikabili Burundi utapatiwa ufumbuzi haraka iwezekanavyo. Kabla ya kufanya mazungumzo na Rais wa Burundi, mkuu wa kundi la usuluhishi katika mzozo wa Burundi alikuwa ameshafanya mazungumzo pia na Marais wa Uganda na Rwanda.
Benjamin Mkapa amesema kuhusiana na hitilafu kati ya Burundi na Rwanda kuwa, nchi za Kiafrika ni wanachama wa taasisi moja, na kwamba nchi hizo zikiwa majirani zinapaswa kushirikiana na kuishi katika mazingira ya amani, utulivu ili kuimarisha ustawi wa kiuchumi kwa pamoja.
Wakati huo huo machafuko nchini Burundi yangali yanaendelea. Siku chache zilizopita miripuko kadhaa ilitokea katika maeneo tofauti nchini humo na kuuwa na kujeruhi watu kadhaa. Naibu Msemaji wa polisi ya Burundi juzi alitangaza kuwa wanajeshi wanne wa nchi hiyo walishambuliwa na kujeruhiwa na watu waliokuwa na silaha wakati wanajeshi hao walipokuwa kwenye doria katika eneo la Musaga kusini mwa Bujumbura mji mkuu wa Burundi. Aidha watu wasiopungua watatu walijeruhiwa katika miripuko miwili ya guruneti huko Mutanga kaskazini mashariki mwa Bujumbura. Miripuko hiyo imetekelezwa siku mbili baada ya kuuliwa Darius Ikurakure na Didier Muhimpundu maafisa wawili wa jeshi la Burundi.
Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa wiki iliyopita liliitisha kikao kujadili hali ya mambo ya Burundi. Katika kikao hicho, taasisi zisizo za kiserikali za nchi wanachama wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa ziliitaka serikali ya Burundi ianzishishe mchakato wa mazungumzo ya kisiasa kati yake na wapinzani.