SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumamosi, 12 Machi 2016

T media news

Mkwamo mwingine wa kisiasa nchini Lebanon, hitilafu kuhusu sheria ya uchaguzi

     
Mkwamo mwingine wa kisiasa nchini Lebanon, hitilafu kuhusu sheria ya uchaguzi
Huku hitilafu baina ya makundi ya kisiasa ya Lebanon kuhusu mtu wa kuchukua nafasi ya rais iliyo wazi kwa miaka miwili sana zikiendelea, kamati ya watu tisa ya kutunga sheria mpya ya uchaguzi nchini humo imeshindwa kuafikiana kuhusu sheria hiyo.
Kamati ya bunge ya watu tisa ya kutunga sheria mpya ya uchaguzi nchini Lebanon inapaswa kutoa ripoti yake ya mwisho siku ya Jumanne ya tarehe 15 Machi na kuikabidhi kwa Spika wa Bunge la nchi hiyo. Hata hivyo habari zinasema kuwa, licha ya kupita miezi mwili na nusu tangu kamati hiyo ianze kazi ya kutunga sheria mpya ya uchaguzi, wajumbe wake wameshindwa kufikia mwafaka kuhusu ripoti yao ya mwisho. Mikwamo ya kisiasa nchini Lebanon si michache. Tukianza na miezi ya hivi karibuni, zoezi la kuundwa Baraza la Mawaziri la Tammam Salam lilikwama kwa muda wa miezi 11. Sababu kuu ya mkwamo huo ni makundi ya kisiasa ya Libanon ambayo yalitofautiana kuhusu watu wa kuchukua nafasi za mawaziri. Hata baada ya kuundwa baraza hilo la mawaziri, haukupita muda mrefu ila Lebanon ilitumbukia kwenye mkwamo mwingine wa kisiasa uliohusiana na kuchaguliwa mtu wa kushika nafasi ya rais Michel Sulaiman aliyemaliza muda wake. Kipindi cha urais wa Michel Sulaiman kilimalizika mwezi Mei 2014, lakini hadi hivi sasa miezi 22 imepita na hakuna rais mpya aliyechaguliwa. Hitilafu za mitazamo baina ya makundi ya kisiasa nchini Lebanon ni kubwa mno kiasi kwamba hata haiwezekani kujua watu waanzie wapi ili kuzitatua. Katika kipindi cha miezi 22 iliyopita, kumepangwa kufanyika vikao 35 vya Bunge, lakini kilichofanyika ni kikao kimoja tu, huku vikao vyote 34 vingine vikishindwa kufanyika kutokana na kutotimia akidi. Lebanon imepitisha miezi 22 bila ya kuwa na Rais katika hali ambayo kwenye kipindi hicho chote imekuwa na matatizo ya kila namna, kuanzia matatizo ya kiusalama hadi mashinikizo ya kieneo hususan kutoka kwa Saudi Arabia. Hivi sasa pia inaonekana kuwa, suala la kupata sheria ya uchaguzi limekwama. Siku chache tu zimebakia hadi kumalizika muda wa kazi za kamati ya kutunga sheria ya uchaguzi yaani siku ya Jumanne ya tarehe 15 Machi, lakini hadi hivi sasa hakuna matumaini ya kupatikana mwafaka baina ya wajumbe wa kamati hiyo ya bunge kuhusu sheria hiyo. Wachambuzi wa mambo wanatabiri kuwa, Lebanon iko mbioni kutumbukia kwenye mkwamo mwingine wa kisiasa. Wanasema kuwa, kama ambavyo Lebanon imekwama katika kuainisha Rais wa nchi hiyo kutokana na matatizo yaliyomo kwenye sheria ya kuchagua rais, ni vivyo hivyo itakumbwa na tatizo jingine katika uchaguzi wa wabunge, karibuni hivi. Kuongezeka masuala yanayopelekea kuzidi kushuhudiwa mkwamo wa kisiasa nchini Lebanon ni uthibitisho wa wazi kuwa nchi hiyo inahitajia kuwa na mtazamo mpya wa kisiasa na kisheria kuhusu namna ya kuchagua rais, namna ya kufanya uchaguzi wa bunge na hata suala la kuteua Waziri Mkuu.