KONGAMANO la Kikanda la Viongozi Wastaaafu wa Afrika limeazimia mambo makuu matano ikiwamo la kuwataka viongozi walio madarakani kuimarisha mifumo yao ili kusaidia kulinda amani na kuzuia migogoro.
Kongamano hilo lililoongozwa na Rais mstaafu wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa, lilihudhuriwa na Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, Rais mstaafu wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud na washiriki wengine kutoka taasisi za kitaifa, kikanda na kimataifa zinazojihusisha na masula ya usalama na kulinda amani.
Akisoma mazimio hayo jana jijini Dar es Salaam, Mwakilishi wa chuo cha Uongozi, Gerase Kamugisha, alitaja maazimio hayo kuwa ni kuimarisha taasisi za kanda na Umoja wa Afrika zenye jukumu la kujenga na kulinda amani.
Alitaja aazimio lingine kuwa ni kuongeza uratibu, ushirikiano na mashauriano miongoni mwa taasisi za kitaifa, kikanda na bara zima zinazohusika na juhudi za kuzuia migogoro au kulinda amani ikiwamo kuimarisha mifumo ya ushirikiano baina ya Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika (AU) na Baraza la Umoja wa Mataifa ili kuongeza sauti ya Afrika katika maamuzi ya Umoja wa Mataifa kuhusu amani na usalama wa Afrika.
Mengine ni kuhakikisha nchi zote wanachama wa Umoja wa Afrika zinajiunga na kutumia mfumo wa kujitathmini wa Afrika (APRM) kama chombo muhimu cha kuimarisha maridhiano ya kitaifa na kuzuia migogoro, uvunjifu wa amani na kuhamasisha serikali kushiriki kugharamia shughuli za kulinda amani.
Kamugisha alisema kongamano la kikanda la viongozi wastaafu wa Afrika kuhusu nafasi ya Afrika katika mfumo wa amani na usalama ulimwenguni lilifanyika Mei 17, mwaka huu jijini.
Alisema kongamano hilo ni mwendelezo wa kongamano ambalo lilifanyika Johannesburg, Afrika kusini Agosti mwaka jana.
“Katika kongamano hilo, viongozi walianzimia kuendeleza mjadala wao kwa kuangalia kwa kina zaidi suala la nafasi ya Afrika katika mifumo ya usimamizi wa amani na usalama ulimwenguni,” alisema
Aidha, alisema ili kujenga mazingira ya uhalisia, kongamano limetumia hali halisi ya nchi ya Somalia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kama mifano halisi inayotoa mafunzo kwa ajili ya mjadala wa kongamano.
Kamugisha alisema mwenyeji wa kongamano hilo alikuwa Rais mstaafu Mkapa na waliohudhuria ni rais mstaafu wa Afrika Kusini Thabo Mbeki na rais mstaafu wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud na washiriki wengine walitoka katika taasisi za kitaifa, kikanda na kimataifa zinazojihusisha na masula ya usalama na kulinda amani.