Afisa Habari wa Klabu ya Simba, Haji Manara amefunguka na kuwataka mashabiki wa wekundu Msimbazi kutoangaishwa wala kuhuzunika na matokeo mabaya waliyoyapata dhidi ya Stand United na kudai hicho sio kigezo cha kupotea katika ligi.
Manara ametoa kauli hiyo leo (Machi 03, 2018) wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari makoa makuu ya klabu hiyo eneo la Kariakoo Jijini Dar es Salaam na kusema sare ya mabao waliyoipata katika mchezo wa jana imekuwa ishara tosha ya kuzidi kujiweka sawa katika michezo mingine inayokuja mbele yao.
"Msiangaishwe na matokeo ya mchezo wetu dhidi ya Stand United 'that is football', kuna vitu hutokea kwa sababu ya mipango ya Mungu, kwangu mimi tungeshinda jana (Ijumaa) ingekuwa 'much better' lakini kutoka sare kabla ya kuja kucheza na waarabu imekuwa kama ishara kwetu ya kuwa makini katika mchezo huo", amesema Manara.
Pamoja na hayo, Manara ameendelea kwa kusema "kama tungefunga mabao 5 au 6 mashabiki zetu wangeona mechi na Al Masry kutoka nchini Misri nayo ni rahisi tu. Vitu vingine vinakuja kwa mipango yake mwenyewe Mwenyezi Mungu, kwa hiyo niwaombe mashabiki msiangaishwe wala kuhuzunika sana kuona tumeshapotea katika ligi".
Kwa upande mwingine, Klabu ya Simba inatarajia kucheza mchezo wake wa Kombe la Shirikisho dhidi ya klabu ya Al Masry kutoka nchini Misri siku ya Jumatano (March 7,2018) katika uwanja wa Taifa Jijini Dar es salaam huku viingilio vya mchezo huo vikiwa ni VIP A- Tsh 20,000, VIP B- Tsh 15,000 na mzunguko shilingi 5,000.