Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Kilimanjaro, kimechukua uamuzi wa kuumsimamisha Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa chama hicho (BAVICHA), Dickson Kibona ili kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili.
Kibona alisimamishwa uongozi Februari 28, mwaka huu ikiwa ni siku 11 tu zimepita tangu kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa marudio ya ubunge katika jimbo la Siha ambapo CHADEMA iliangushwa na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Katika taarifa iliyotolewa jana na Katibu wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa ilieleza kwamba ilimwandikia kibona barua kuchukua hatua ya kinidhamu sehemu ya kazi kuhusu tuhuma zinazomkabili kama kiongozi na kama mwanachama wa chama hicho.
“Ofisi ya Chadema Kanda ya Kaskazini, ambayo ni mamlaka ya nidhamu na uwajibishaji kwa viongozi wa mikoa, ilimwandikia barua Kibona ambaye ni Mratibu wa Bavicha Kilimanjaro, kwa mujibu wa ibara ya 6.5.2 ya kanuni za chama ya utaratibu wa kuchukua hatua ya kinidhamu sehemu ya kazi kuhusu tuhuma zinazomkabili kama kiongozi na kama mwanachama wa Chadema,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa maelekezo hayo ya Golugwa ambayo yanasema kwa uzito na unyeti wake, Ofisi ya Kanda imeelekeza Kibona kusimama na kupisha uchunguzi.
Imeeleza kuwa hatua hiyo ni ya kiutawala na itatoa fursa kwa kipindi ambacho Kibona ameelekezwa kwenye barua aliyopewa kujibu tuhuma kuhusu ama aachishwe uongozi au afukuzwe uanachama kwa mujibu wa ibara ya 6.3.4 (b) na (c).