SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumamosi, 19 Agosti 2017

T media news

Polisi Waapa Kuwasaka na Kuwanasa Waliomuua Wayne Lotter Ambaye Ndiye Aliyefanikisha Kukamatwa kwa Malkia wa Meno ya Tembo

Jeshi la Polisi limesema linafanya uchunguzi kuhakikisha linawatia mbaroni watu waliompiga risasi na kumuua Mkurugenzi na Mwanzilishi-Mwenza wa Shirika lisilo la kiserikali la PAMS Foundation, Wayne Lotter jijini Dar es Salaam juzi.

Lotter ndiye aliyefanikisha kukamatwa kwa mfanyabiashara kinara wa meno ya tembo, Yang Feng Glan maarufu kama ‘Malkia wa Meno ya Tembo’ hivi karibuni baada ya mhalifu huyo kusakwa kwa muda mrefu katika mataifa mbalimbali duniani.

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limesema linafanya upepelezi wa hali ya juu ili kuhakikisha kuwa linawatia mbaroni wahusika wa mauaji hayo huku Waziri wa Maliasili na Utalii Profesa Jumanne Maghembe akieleza kusikitishwa na tukio hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Kamanda Kanda Maalumu, Lucas Mkondya alisema tukio hilo lilitokea Agosti 16, saa tano maeneo ya makutano ya barabara ya Haile Selassie na Kaole eneo la Masaki.

Taarifa kutoka eneo la tukio zinasema Lotter (51), alipigwa risasi katika maeneo hayo ya Masaki, wakati akitokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) ambapo teksi aliyopanda ilisimamishwa na gari lingine kabla ya watu wawili kutelemka na kumpiga risasi.

Lotter alikuwa Mkurugenzi na Mwanzilishi-Mwenza wa PAMS Foundation, Shirika lisilo la Kiserikali ambalo linajihusisha na masuala ya kupinga ujangili ambalo lilianza shughuli zake Tanzania mwaka 2009.

Imeelezwa kuwa Lotter amekufa huku akiwa amepanga kufanya mikakati mbalimbali ya kukabiliana na ujangili wa tembo ikiwemo kuzindua vilabu vya kupinga ujangili, kufunga vifaa vya GPS kwa tembo wote nchini, pia alikuwa msaada kwa serikali kupitia miradi mbali mbali kama vile kufanikisha kumkamata malkia wa ndovu aliyekuwa anatafutwa Dunia nzima ambaye alikamatwa nchini miezi michache iliyopita.

Pia alianzisha vikosi vya ulinzi (game rangers) ambao aliwalipa ili kusaidia ulinzi wa tembo kwenye mbuga mbalimbali nchini. 

Alifadhili pia filamu ya The Ivory Game iliyochezewa Tanzania na China, ambayo ilizinduliwa Hollywood, Marekani ikionesha ujangili unavyofanyika na pia alisaidia magari ya doria kwa Jeshi la Polisi na Wizara ya Maliasili na Utalii.

Kamanda Mkondya alisema wauaji hao wanaodhaniwa kuwa ni majambazi mbali na kumuua mkuregenzi huyo, walipora kompyuta mpakato tatu, simu moja aina ya Nokia na nyaraka mbalimbali 

Alisema marehemu alikuwa akitokea mkoani Arusha akiwa amepanda gari ya kukodi yenye namba za usajili T 499 DEV aina ya Toyota Sienta pamoja na mfanyakazi mwenzake, Christine Clarkl (40) raia wa Afrika Kusini.

Mkondya alisema raia hao walikuwa wanaelekea Bawbaw Apartment zilizoko maeneo ya barabara ya mwaya Masaki kwa ajili ya mapumziko ambapo wakiwa njiani alitokea mtu mmoja akiwa na gari na kuwaziba kwa mbele akiwa amevaa koti jeusi na baadaye alifyatua risasi mbili akidai apewe dola ambapo risasi ilimjeruhi marehemu mdomoni na baadaye alifariki dunia akiwa anapelekwa Hospitali ya Sami iliyopo Masaki kwa ajili ya kupatiwa matibabu.