Kufatia kikao kilichoendeshwa na kamati ya utendaji ya CAF, huko Addis Ababa, kamati hiyo imetangaza kuwa, Franceville pamoja na Port Gentil itakuwa ni miji ambayo yatachezwa mashindano ya AFCON U17 kuanzia May 14-28.
Mashindano hayo yatakayofanyika kwa wiki mbili awali yalipangwa kuanza May 21 hadi June 4 lakini ratiba imerudishwa nyuma kwa wiki moja na yataenda sambamba na michuano ya kombe la Dunia kwa vijana FIFA U20 ambayo yataanza May 20 – June 11 huko Korea Kusini.
Hayo ni matokeo ya CAF kuhamisha mashindano hayo kutoka Madagascar ambapo serikali ilishindwa kuthibitisha kuandaa mashindano ya AFCON U17 na kulazimika kupelekwa Gabon baada ya nchi hiyo kuibwaga Sudan katika kinyang’anyiro cha nchi itakayoandaa mashindano hayo.
Miji yote ilitumiwa wakati wa michuano ya AFCON 2017 kuanzia January 14 hadi February 7 ambapo Kundi B lilikuwa mashariki mwa jiji la Franceville huku Kundi D likiwa kwenye jiji lenye utajiri mkubwa wa mafuta Port Gentil.
Stade de Franceville na Stade de Port Gentil kwa pamoja ni viwanja ambavyo vinauwezo wa kubeba mashabiki 20,000. Wenyeji Gabon, Cameroon, Guinea na Ghana wapo Kundi A wakati mabingwa watetezi Mali, Angola, Niger na Tanzania wakiwa wao wapo Kundi B.