Msanii wa Bongo fleva, mwanadada Kadjanito aliyewahi kutamba na ngoma yake ya Maumivu, amefunguka na kusema kuwa tangu aoelewe, kitu anachotamani zaidi kupata ni ujauzito.
Kadjanito ambaye tangu afunge ndoa amebadili jina na kuitwa Natasha Lisima, ametoa kauli hiyo akiwa katika kipindi cha FNL kinachoruka kila Ijumaa saa 3 usiku, na kufafanua kuwa kwa sasa bado hajabarikiwa kupata lakini akiupata atafurahi sana.
"Mtoto kwa sasa bado, lakini nikipata ujauzito nitafurahi sana, nitatembea tumbo mbele, hata Mungu alisema zaeni mkaongezeke" Amesema Natasha.
Kuhusiana na maisha yake mapya ndani ya ndoa, Natasha anasema amefurahi kupata mwanaume mwenye kila sifa anayoitaka, na kwamba hafikirii kuachana naye hata iweje kwa kuwa anampenda sana.
"Mume wangu ni mchezaji wa mpira wa miguu na ni mkongo, kwahiyo hana makazi maalum, lakini ni muelewa sana, popote pale atakapokuwa tutaishi ,naamini tutaendelea kudumu kwa maisha yetu yote, maisha yangu ya ndoa hayaingiliani na kazi yangu" Amesema Natasha na kuongeza kuwa kuanzia sasa hataki tena kuitwa Kadjanito bali Natasha Lisima kwa kuwa amebadili dini ili kufunga ndoa na mpenzi wake huyo anayeitwa Lisima.
Kuhusu muziki, Natasha amesema kuwa kuingia kwenye ndoa hakutamuathiri kwenye muziki, na kwamba ataendelea na muziki kama kawaida huku akiahidi kutoa ngoma mpya mwishoni mwa mwezi huu huku akiweza wazi kuwa haogopi wala hatishwi na ujio wa wasanii wengine wa kike kwenye game.