Mshambuliaji wa Simba Musa Hassan Mgosi ambaye August 14, 2016 aliamua kulipa kisogo soka la ushindani, ametaja nyakati tofauti ambazo amewahi kufurahi na kuhuzunika akiwa kama mchezaji wa Simba.
Yanga ni moja ya timu ambazo zimewahi kumfanya Mgosi ahuzunike katika maisha yake ya soka akiwa kama mchezaji wa Simba.
“Yapo mambo mengi ambayo siwezi kuyasahau katika soka, nyakati za furaha na huzuni. Kitu ambacho nimewahi kukifurahia nikiwa Simba ni siku nilipocheza mechi yangu ya kwanza ilikuwa kwenye mashindano ya Tusker. Ilikuwa ni mechi kubwa kwangu kwasababu ilikuwa ni mechi ya kwanza kwangu nikiwa Simba halafu ilikuwa ni nusu fainali lakini niliweza kufunga magoli mawili na tukawatoa Villa,” alisema Mgosi mara baada ya kustaafu soka kwa heshima katika klabu ya Simba.
“Mechi ambazo zimewahi kunipa majonzi ni mechi za watani wa jadi (Yanga) kutufunga mara mbili mfululizo kwenye msimu uliopita kitu ambacho hakijawahi kutokea katika maisha yangu ya mpira tangu nimejiunga Simba.”
Msimu uliopita Simba ilikubali vichapo viwili katika raundi zote za ligi kuu Tanzania bara kwa vipigo vya magoli mawili katika kila mechi na kuacha pointi sita zikienda Jangwani.
“Nawashuru wanachama, mashabiki na viongozi wa Simba wameniamini kwa muda mrefu na nathamini mapenzi yao kwangu na mimi nimefanya kazi kwa kila kitu ambacho nilitakiwa kukifanya wakati nikiwa mchezaji wa Simba, kilichobaki kwasasa ni ushirikiano ili tusukume gurudumu mbele kile wanachokitaka basi wachezaji wakitekeleze.”
Klabu ya Simba imemteua Mgosi kuwa team Manager wa klabu ya Simba na ataendelea kuonekana kwenye benchi la ufundi la ‘Wekundu wa Msimbazi’ licha ya kuamua kutundika daruga.