WAKATI serikali ikijiandaa kuhamia Mkoa wa Dodoma, Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa imebaini kuwepo kwa madudu katika Sekretarieti ya mkoa huo, anaandika Dany Tibason.
Kamati hiyo imebaini kuwepo kwa matumizi mabaya ya fedha za serikali ikiwa ni pamoja na kujiuzia magari ya serikali bila kufuata utaratibu.
Japhet Hasunga, Mwenyekiti wa Kikao cha Kamati ya PAC ambaye ni Mbunge wa Vwawa (CCM) amesema, watumishi wamekuwa wakijiuzia magari ya serikali, wakipeana pia wakiyatengeneza katika gereji bubu.
Mbali na hayo pia kuna sintofahamu kuhusu ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambao kamati hiyo imehoji sababu ya kununuliwa kwa vifaa vipya wakati jengo halijakamilika.
Kutokana na kuwepo kwa madudu hayo katika Sekretalieti ya Mkoa wa Dodoma, PAC imetoa maagizo saba kwa uongozi wa mkoa kutokana na kushindwa kujibu hoja kutokana na Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG).
Hasunga ameagiza mambo saba; kwanza, kamati imeitaka idara ya usimamizi wa mali za serikali kufanya uhakiki maalum wa mali za serikali katika fungu 72 hasa magari yanayofanya kazi, yaliyoharibika na yaliyouzwa na kuwasilisha taarifa ya uhakiki huo maalumu kwa kamati ndani ya miezi mitatu.
Amemtaka Ofisa Masuhuri kusimamia kitengo cha uhasibu ili kuzingatia viwango vya kimataifa ya utayarishaji wa mahesabu katika utayarishaji wa mahesabu ya serikali ili kuepuka hati za ukaguzi zenye dosari.
Akitoa maagizo amesema, kamati inamwagiza Ofisa Masuhuri kuzingatia sheria ya manunuzi ya mali ya umma na kanuni zake katika shughuli za sekretalieti ikiwa ni pamoja na kupata vibari kwenye mamlaka husika anapofanyika uhamisho wa fedha katika vifungu mbalimbali.
Mbali na hilo kamati imemuomba CAG kwa kushirikiana idara ya mali za serikali kufanya tathimini ya kina kuiridhisha kamati iwapo garama za Sh. 12.5 Mil zilizotumika katika ujenzi wa jengo la ofisi ya mkuu wa mkoa kama zinakidhi thamani halisi ya sasa.
Hasunga pia ametoa agizo la tano kuwa Ofisa Masuhuri awasilishe taarifa ya maandishi kuhusu matumizi ya kiasi cha Sh. 665.3 Mil na chanzo cha fedha hizo kabla ya muda wa kazi kesho.
Ofisa huyo ametakiwa kuwasiliana na Ofisi ya Rais Utumishi ili kuhakikisha nafasi za kazi zinazokaimiwa zinajazwa mapema iwezekanavyo ili kuongeza ufanisi wa sekretalieti katika Mkoa wa Dodoma.
Agizo la saba lililotolewa na PAC kwa Mkoa wa Dodoma amesema, kwa kuwa hoja nyingi za ukaguzi bado hazijapata majibu sahihi, kamati kamati inatoa muda wa miezi sita kwa sekretarieti kukamilisho hoja za kukaguzi na taarifa ya utekelezaji ziwasilishwe kwa CAG na kwa kamati kabla ya miezi sita kuisha.