SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatatu, 8 Agosti 2016

T media news

Aleppo, mtihani wa kifo na uhai kwa makundi ya kigaidi

Jeshi la Syria likijitayarisha kukomboa kikamilifu mji wa Aleppo

Mji wa Halab (Aleppo) ambao wakati mmoja ulikuwa mji mkuu wa kiuchumi wa Syria hii leo umekuwa uwanja wa kujipima misuli makundi ya kigaidi kwa ajili ya kubakia na kuendelea kuwepo nchini humo.

Makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na nchi kama Marekani, Saudi Arabia na Uturiki zinayoyaita eti yenye misimamo ya wastani, hivi sasa yanazingirwa na jeshi la Syria na wapiganaji wa Hizbullah katika mji huo. 

Jeshi la Syria katika mitaa ya Aleppo

Mji wa Halab ambao ni wa pili kwa ukubwa nchini Syria umekuwa ukishuhudia mapigano makali tangu mwaka 2012 na tangu Julai mwaka huu maeneo yake ya mashariki, kusini na kusini magharibi yanazingirwa na jeshi la Syria na waitifaki wake. Baada ya magaidi walioko katika mji huo kuzingirwa, nchi za Magharibi zinazodai kipambana na ugaidi sasa zinapaza sauti juu na kudai kuwa, serikali ya Syria ikishirikiana na Russia zinafanya hila huko Aleppo katika fremu ya kutoa misaada kwa raia waliokwama katika mapigano makali kwenye mji huo. 

Sambamba na hayo Rais Bashar Assad wa Syria ametangaza msamaha kwa mtu yeyote atakayeweka chini silaha na kujiunga na wananchi. Baada ya tangazo hilo mamia ya wapiganaji wa makundi hayo wamejisalimisha kwa jeshi la Syria. Hatua hiyo imewakasirisha sana waungaji mkono wa makundi ya kigaidi yanayodaiwa kuwa yenye misimamo ya wastani na sasa nchi za Marekani, Saudi Arabia na wenzao wanafanya jitihada kubwa za kuimarisha kambi ya magaidi katika mji wa Aleppo.

Magaidi wanashambulia makazi ya raia Aleppo 

Makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na Marekani, Saudi Arabia na Uturuki nchini Syria sambamba na kufanya mashambulizi ya makombora na mabomu dhidi ya maeneo ya raia katika mji wa Aleppo kwa ajili ya kuvunja mzingiro wa jeshi la Syria, yanafaidika pia na ripoti na taarifa za kiintelijensia za ndege za kijasusi za waungaji mkono wao. Suala hilo limekuwa sababu ya kushadidi zaidi mapigano ya Jumamosi na Jumapili ya jana katika mji huo. 

Jana Jumapili jeshi la Syria lilifanikiwa kudhibiti njia ya kutuma wapiganaji zaidi kwenye maeneo ya vita. Kwa sasa makamanda wa makundi hayo ya kigaidi wanafanya jitihada za kuondoka katika maeneo yanayozingirwa na jeshi la Syria katika mji wa Aleppo na kuweza kuwatorosha maafisa wa kijeshi wa nchi za Uturuki, nchi za Kiarabi na hata zile za Magharibi wanaoshirikiana na magaidi hao. 

Hali, kama vinavyotangaza vyombo vya habari vya nchi zinazowaunga mkono magaidi huko Syria, ni ngumu sana kwa makundi ya kigaidi yaliyopo katika mji wa Aleppo na wapiganaji wa makundi kama lile linalojiita Jeishul Fat'h yako chini ya mashambulizi makali ya jeshi la Syria.

Mapigano makali yanaendelea Aleppo

Mji huo sasa umekuwa medani ya mpambano mkali kati ya waungaji mkono wa makundi ya kigaidi na safu za muqawama na mapambano ya ukombozi na huo ni utangulizi wa kuufanya tena mji huo kuwa ngome ya kwanza ya wapiganaji wa mstari wa mbele wa kupambana na adui nambari moja wa ulimwengu wa Kiislamu yaani utawala haramu na bandia wa Israel.

Ushindi wa jeshi la Syria na waitifaki wake katika vita vya Aleppo utakuwa mwisho wa kuwepo makundi ya kigaidi nchini humo na hapana shaka kuwa, mafanukio hayo yatakuwa na taathira kubwa katika mustakbali wa eneo zima la Mashariki ya Kati.            

Aug 08, 2016 07:50 UTC