SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 29 Juni 2016

T media news

Wabunge Wataka CUF Ifutiwe Usajili


MBUNGE wa Viti Maalum (CCM), Munira Mustafa Khatib, ameitaka serikali kukifutia usajili Chama cha Wananchi (CUF), kwa madai kuwa kimekuwa kikishiriki katika matukio ya kupigwa na kuharibu mali za wananchi visiwani Pemba.

Mbunge huyo alitoa kauli hiyo jana, alipokuwa akiuliza swali la nyongeza katika kipindi cha maswali na majibu bungeni.

 

“Kutokana na kuwapo matukio ya wananchi kupigwa hususan wanachama wa CCM, ni kwanini serikali isikifutie usajili chama cha CUF kwakuwa ndio chanzo cha matukio hayo visiwani pemba,”alihoji Mbunge huyo.

 

Katika swali la Msingi la Mbunge wa Chambani (CUF), Yusufu Salim Hussein, naye alihoji kama serikali inatambua tatizo la raia kupigwa na kuharibiwa mali zao kwa upande wa Zanzibar, ambalo limekuwa likiongezeka siku hadi siku na hatua gani zimechukuliwa.

 

Kutokana na masuala hayo, wabunge walionekana wakisimama kuuliza maswali ya nyongeza na Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Tauhida Cassian Nyimbo, alihoji serikali inachukua hatua gani kwa viongozi wa CUF ambao wamekuwa wakitoa kauli za vitisho kupitia mitandao ya kijamii na kuwafanya wananchi visiwani humo kuwa na hofu hasa kipindi hichi cha kuelekea sikukuu ya Idd el Fitri.

 

Naye Mbunge wa Dimani (CCM), Hafidh Ali Tahir, alihoji ni kwa namna gani serikali itawashughulikia baadhi ya viongozi ambao wamekuwa na tabia ya kuvunja sheria na maagizo ya viongozi kuhusu mikutano ya hadhara.

 

Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni, alisema serikali inatambua kwamba kila unapofika wakati wa Uchaguzi Mkuu hasa katika kisiwa cha Pemba, baadhi ya watu hujichukulia sheria mkononi kwa kuwapiga wengine na kuharibu mali zao.

 

Kutokana na hali hiyo, alisema serikali itaendelea kuongeza vikosi vya ulinzi na usalama katika maeneo yote tete na kuhakikisha utii wa sheria bila shuruti unazingatiwa.

 

“Pia serikali itaendelea kuwaelimisha wananchi madhara ya kujichukulia sheria mikononi dhidi ya wengine wasio na hatia,” alisema Masauni.

 

Alitoa wito kwa wananchi wote kuacha mihemko ya itikadi za kisiasa wakati na kabla ya uchaguzi kwani hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

 

Kuhusu viongozi wanaokiuka maagizo ya serikali kuhusu mikutano ya kisiasa, Masauni alisisitiza mikutano hiyo haitakiwi kwa wakati huu hadi hapo polisi itakapoona inafaa na kuvitaka vyama vya siasa kutii maagizo ya serikali.

 

“Hakuna mtu ambaye yuko juu ya sharia. Wale watakaoleta ukorofi watachukuliwa hatua kali bila kujali kama ni kiongozi wa aina gani na mahali gani anatokea. Lazima sheria ichukue mkondo wake,”alisema.

 

Kuhusu suala la kukifuta CUF, Naibu Waziri huyo alisema jukumu hilo si la serikali bali limo mikononi mwa Msajili wa vyama vya siasa, ambaye anatakiwa kuliangalia kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo.

 

Aidha, alisema nchi iko salama na serikali itaendelea kuhakikisha amani na utulivu vinakuwapo wakati wa sikukuu hiyo na kuwataka wananchi kupuuza kauli za uchochezi zinazotolewa na wanasiasa.

 

Baada ya kipindi hicho, Mbunge wa Mwibara, (CCM), Kangi Lugola, aliomba mwongozo kwa Naibu Spika akisema ni kwa nini serikali ipo bungeni; isitoe majibu kuhusiana na matukio yanayofanywa na CUF ambayo mbunge mwenzake amependekeza kifutiwe usajili na badala yake inatoa jukumu kwa msajili wa vyama vya siasa wakati ni sehemu ya serikali.

 

Kutokana na mwongozo huo, Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, alisema atatoa majibu ya mwongozo huo baada ya kupitia sheria ya vyama vya siasa inasemaje.