SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 29 Juni 2016

T media news

Vita kumrithi David Cameron yapamba moto


Anayetaka kugombea kupitia chama tawala cha Conservatives cha nchini Uingereza, Stephen Crabb.

Na Leonard Msigwa

VITA ya kuwania uongozi wa juu ndani ya chama tawala cha Conservatives cha nchini Uingereza, imeanza kushika kasi. Wanasiasa mbalimbali wenye nguvu na uwezo wameonyesha nia ya kutaka kumrithi waziri mkuu aliyejiuzulu, David Cameron.

Steveb Crabb amekuwa mwanasiasa wa kwanza kujitokeza hadharani na kutamka nia yake ya kutaka kuirithi nafasi hiyo. Crab ameweka bayana kwa kusema kwamba: “Najitokeza kuwania nafasi ya kiongozi wa juu ndani ya chama na baadaye kuwa waziri mkuu. Naipenda nchi yangu, nakipenda chama changu”.

Mwanasiasa huyo alijiunga na Conservative mara tu alipohitimu elimu yake ya chuo kikuu. Alianza siasa rasmi 1998 alipochaguliwa kama mwenyekiti wa chama cha Southwark North and Bermondsey Conservative Association, nafasi aliyodumu nayo hadi mwaka 2000.

Mwaka 2001 aligombea ubunge jimbo la Preseli Pembrokeshire ambako alishika nafasi ya pili. Aligombea tena mwaka 2005 na kuwa mbunge kijana zaidi huku akikigaragaza chama cha Labour kilichoshikilia jimbo hilo kwa muda mrefu. Mwaka 2010 na mwaka 2015 aligombea na kushinda kwa kura nyingi zaidi katika nafasi anayoitumikia hadi sasa.

Vilevile alikuwa msaidizi wa waziri mkuu aliyestaafu akitumikia nafasi ya katibu wa baraza la mawaziri kitengo cha mafao na kazi. Ameweka wazi hatojiuzulu nafasi yake na nia yake ni kugombea uongozi ndani ya chama chake na taifa kwa ujumla.

Alipoulizwa na waandishi wa habari kwa nini ameamua kujitokeza hadharani kuwania nafasi hiyo nyeti zaidi nchini humo, alisema, “Nina wasiwasi sana na mustakabali wa baadaye wa nchi yetu iliyogawanyika, mimi ni mtu pekee wa kuiunganisha tena Uingereza”.

Crabb ni mmoja wa washirika wa karibu wa Cameron na anayejivunia kufanya kazi kwa karibu na waziri huyo aliyestaafu. Ameandika kwenye kolamu ya gazeti maarufu la Daily Maily kwamba: “Hatuwezi kukubali kuona raia wetu wanazidi kugawanyika kwa kuitana majina ya kututenganisha ya ‘Remainer’ na ‘Brexit’ (yakimaanisha waliotaka kubaki na waliotaka kujitoa katika Umoja wa Ulaya),  lazima tuungane sote kama taifa’.

Ni dhahiri taifa la Uingereza linamhitaji mtu muhimu wa kuwaunganisha tena Waingereza ambapo Crabb amejipambanua wazi kuwa na nia na malengo ya kuwaunganisha tena Waingereza baada ya kugawanyika. Lakini hawezi kutimiza ndoto hiyo ya kuwaunganisha Waingereza kama hataweza kuwashawishi wanachama wenzake wa Conservative kumchagua kuwa kiongozi wao.

Alikuwa akipinga suala la Uingereza kujitoa kutoka Jumuiya ya Ulaya, ila kwa sasa anasema maamuzi ya wengi ndiyo ya kufuata,“nataka kuiongoza serikali ambayo itayafanyia kazi maoni ya walio wengi. Nataka kutimiza matarajio ya wananchi milioni kumi na saba waliopiga kura ya kujitoa kwenye jumuiya. Ni wakati wa kuipitia tena sera yetu ya uhamiaji, uhuru wa kuingia nchini mwetu katika njia bora ya kuimarisha usalama wetu”.

Watu wengi wanatajwa kuwania kumrithi Cameron, hivyo kujitokeza hadharani kwa Crabb ni wazi sasa joto la uchaguzi nchini Uingereza limepamba moto. Septemba mwaka huu wanachama wa Conservative wataamua nani mrithi halali wa Cameron.