Hakuna kingine anachowaza Diego Simeone wa Atletico Madrid zaidi ya fainali itakayo pigwa kwenye mji wa kihistoria wa Milan nchini Italia. Katika fainali hiyo Diego anaingia akiwa na kisasi cha fainali ya mwaka 2014,Diego anaingia kwenye fainali hii ya sasa akiwa na jeshi kamili huku akiwa amebeba ule msemo unaosema hakuna kitu kitamu kama kisasi “the revenge is sweater than anything”.
Nadhani Simeone alikuwa anasali Real Madrid ili afuzu fainali akakutane naye kwa kulipiza kisasi sababu hakuna muda mwingine wa kucheza dhidi yao zaidi ya sasa.
Safari ambayo amepitia Simeone kuiwezesha Atletico Madrid kufuzu fainali hii si ya kitoto kabisa. Kuanzia kwenye makundi hadi fainali amecheza na timu ambazo zinachangamoto kubwa na historia kwenye soka la Ulaya. Inahitaji moyo wa chuma kufanikisha hayo yote kama wasemavyo kasi ya kiongozi wa wahuni ndio kasi ya wahuni wenyewe. Moyo mgumu wa Simeone umepandikizwa kwa wachezaji wa Atletico Madrid na yeye mwenyewe Diego.
Kumpiga Real Madrid kwenye fainali kutamfanya Diego Simeone aweke historia ya kuzipiga timu tatu bora za dunia mfululizo akianza na Barcelona robo fainali,Bayern Munich nusu fainali na sasa ana msubiri Real Madrid kwenye fainali kubwa ya Ulaya. Akifanikiwa kufanya hilo atasimama mbele ya kamera na kujipiga kifua chake akimanisha yeye ni bingwa wa wote hao.
Atletico Madrid ya sasa ni tofauti na ile iliyocheza fainali mwaka 2014. Hii ya sasa imekuwa na uhakika wa kufunga magoli zaidi ya ile ambayo ilikuwa ngumu zaidi katika kuzuia. Atletico Madrid hii wanaingia uwanjani wakiwa na matokeo ya mchezo kabisa na wanachofanya ni kukamilisha walichopanga. Pia hii ya sasa imejaza damu changa zenye uchu wa mafanikio kuanzia golini hadi mbele kwa washambuliaji.
Sidhani kama Diego Simeone atakuwa na cha kusimulia zaidi ya kuachia hisia zake zizungumze jinsi majaribu hayo magumu alivyo ya shinda sababu hakuna kitu bora zaidi ya kuacha hisia zizungumze zaidi ya maneno.
Furaha kubwa ya Simeone ni kuwaonyesha Real Madrid kuwa hata wao wanaweza bila kuwekeza pesa nyingi kwa wachezaji. Katika vita hii ya fainali Diego anapiga na Zidane ambaye anawasubiri Atletico Madrid alipe kisasi cha kwenye ligi kuu kwa kufungwa pale Santiago Bernabeu. Fainali hii ya sasa imejaa visasi kila upande. Lakini Simeone atakuwa kwenye shambulizi la mwisho kama atafanikiwa kumpiga mpinzani wake.
Ni kama magaidi walivyotungua maghorofa pacha ya Marekani ndivyo Diego Simeone anataka kuitungua Real Madrid kuanzia Zidane,Perez na mashabiki wao. Yeye atatungua maghorofa matatu.